Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Blogu ya Idara ya Habari - MAELEZO

Soko La Madini Chunya Laongeza Mzunguko Wa Fedha Mbeya
Dec 06, 2019
Na Msemaji Mkuu

Tangu kuanzishwa kwake, Serikali yavuna bilioni 8.08
Na Greyson Mwase, Mbeya
Mkuu wa Mkoa wa Mbeya, Albert Chalamila amesema uwepo wa Soko la Madini Chunya lililozinduliwa tarehe 02 Mei, 2019 umepelekea ongezeko la mzunguko wa fedha kwa kuwa wananchi wengi wameanza kushiriki kwenye shughuli za uchimbaji na uchenjuaji wa madini.
Chalamila aliyasema hayo hivi karibuni kupitia mahojiano kwenye maandalizi ya kipindi maalum chenye kuelezea Mafanikio ya Sekta ya Madini, kinachoandaliwa na Tume ya Madini na Wizara ya Madini kwa kushirikiana na Idara ya Habari MAELEZO.
Alisema kuwa,tangu kuanzishwa kwa soko hilo, mabadiliko makubwa yametokea kwenye mkoa wake ikiwa ni pamoja na mzunguko wa fedha kuwa mkubwa na kuongezeka kwa kasi ya uwazi kwenye biashara ya madini.
"Napenda mfahamu ya kuwa, kabla ya kuanzishwa kwa masoko ya madini katika mkoa wa Mbeya, kulikuwepo na changamoto kwenye biashara ya madini kwani wafanyabiashara walikuwa wakifanya kwa kificho kwa kuhofia usalama huku Serikali ikikosa mapato yake stahiki" alisema Chalamila.
Aliendelea kusema kuwa, kwa sasa wafanyabiashara wa madini wanaendesha shughuli zao kwa uwazi kwenye Soko la Madini Chunya huku kodi na tozo mbalimbali za Serikali zikilipwa.
Aliongeza kuwa tangu kuanzishwa kwa Soko la Madini Chunya hadi kipindi cha mwezi Novemba, 2019 Serikali imepata shilingi bilioni 8.08 fedha ambazo zinatumika katika miradi mbalimbali ya maendeleo ikiwa ni pamoja na ujenzi wa barabara, shule, madaraja na vituo vya afya.
Aidha Chalamila aliongeza mabadiliko mengine kuwa ni pamoja na ongezeko la ajira kwenye shughuli za madini na kupunguza wimbi la vijana kukaa vijiweni,  ongezeko la wageni kutoka kwenye mikoa mbalimbali na kukua kwa huduma mbalimbali ikiwa ni pamoja na hoteli, utalii n.k.

Mipangilio
Marekebisho ya Mandhari
Marekebisho ya Maandishi