Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Blogu ya Idara ya Habari - MAELEZO

Singida Waanza Ukaguzi wa Mabasi ya Wanafunzi.
May 18, 2017
Na Msemaji Mkuu

[caption id="attachment_1165" align="alignnone" width="750"] Mkuu wa Kikosi cha Usalama Barabarani mkoani Singida,Mrakibu wa Polisi Peter Majira akitoa taarifa ya zoezi la ukaguzi wa mabasi yanayotumika kusafirisha wanafunzi kwa lengo la kukagua ubora na kuwakumbusha madereva na wamiliki wa mabasi hayo juu ya sheria za usalama barabarani.Ukaguzi huo umefanyika leo Mkoani humo.[/caption]

Na RS- Singida.

Jeshi la Polisi kitengo cha usalama barabarani Mkoa wa Singida limeanza  zoezi kambambe la kukagua mabasi yanayotumika kusafirisha Wanafunzi huku likisisitiza kuwa zoezi hilo litakuwa endelevu.

Akizungumza kwa niaba ya kamanda wa Polisi Mkoa wa Singida, RTO  Mrakibu wa Polisi Peter Raphael Majira, amesema zoezi hilo lililoanza jana litaendelea kwenye Wilaya zote za Mkoa wa Singida.

Amesema Jeshi la Polisi Mkoa wa Singida linatoa elimu na linawakumbusha madereva na wamiliki wa mabasi hayo, juu ya wajibu wao na umuhimu wa kuzingatia kwa umakini mkubwa sheria za usalama barabarani.

  [caption id="attachment_1168" align="alignnone" width="750"] Askari wa usalama barabarani mkoani Singida, E.8763. Sgt. Benes Lucas akikagua mabasi yanayotumika kusafirisha wanafunzi.Ukaguzi huo umefanyika leo Mkoani humo.[/caption]

Aidha, RTO Peter amesema wanawakumbusha madereva kujenga utamaduni wa kuwa na tahadhari zaidi na kitendo hicho kitapunguza kwa kiwango kikubwa ajali za barabarani.

Pia ametumia fursa hiyo kuwataka wenye watoto wanaotumia mabasi hayo wahakikishe mtoto anakaa kwenye kiti chake na si kuchangia kiti.

“Mzazi/mlezi usikubali kabisa mwanao achangie kiti, umelipia kiti kwa nini achangie na wanafunzi mwingine. Na ninyi wamiliki wa mabasi haya kama kuna hafla wanafunzi wanakwenda kuhudhuria iwapo wamejaa  (yaani kila mwanafunzi ana kiti chake), peleka hao waliopata viti halafu urudie wengine” amesisitiza mrakibu Peter.

Kwa upande wao madereva hao wamelipongeza jeshi la Polisi Mkoa wa Singida kwa kuendesha ukaguzi huo na kuwakumbusha juu ya sheria za usalama barabarani.

Mmoja wa madereva wa mabasi ya wanafunzi Mkoani Singida Pyuza Gyumi amesema kwenye mafunzo hayo ya muda mfupi wameagizwa kwamba ni marufuku wanafunzi kuchangia kiti kimoja kwa madai ni ukiukwaji mkubwa wa sheria za usalama barabarani.

“Tumekumbushwa kwamba wakati tukiwa barabarani tuwe makini wakati wote wa kuendesha na tuwe na utulivu wa hali ya juu. Pia tumekumbushwa kuwa makini wakati tunavusha wanafunzi ng’ambo yingine ya barabara. Kwa ujumla binadamu anatakiwa mara kwa mara akumbushwe wajibu wake hii itasaidia kufanya kazi zetu kwa ufanisi”, amesema.

Aidha amesema jeshi la Polisi kuwakutanisha na waajiri wao itasaidia kupunguza kero mbalimbali zinazowakabili kati yao na waajiri wao.

“Kuna wakati tunashindwa kuelewana na matajiri wetu wakati wanapotulazimisha kutenda mambo ambayo ni nje ya sheria za usalama barabarani. Baada ya mafunzo haya ya muda mfupi waajiri wenye tabia hizo watabadilika na kutuunga mkono uzingatiaji wa sheria za usalama barabarani”, amesema Gyumi.

Mipangilio
Marekebisho ya Mandhari
Marekebisho ya Maandishi