Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa amesema Siku ya Wafanyakazi ya Kimataifa (MEI MOSI) ambayo huadhimishwa kila mwaka ni siku maalum kwa ajili ya wafanyakazi kutafakari na kutathmini namna walivyotekeleza malengo waliyojiwekea katika mwaka husika.
Amesema kuwa siku hiyo inatoa fursa kwa wafanyakazi wote duniani kuweka mipango kwa ajili ya mwaka unaofuata na ndiyo maana inafanyika kipindi ambacho nchini nyingi duniani zinakuwa katika maandalizi ya Bajeti.
Amesema hayo leo (Jumatano Mei Mosi, 2024) wakati wa maadhimisho ya Siku ya Wafanyakazi ya Kimataifa inayofanyika kitaifa mkoani Arusha, kwenye uwanja wa Sheikh Amri Abeid ambapo mgeni rasmi katika maadhimisho hayo ni Makamu wa Rais, Dkt. Philip Isdor Mpango ambaye amemwakilisha Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan.
“siku hii ni muhimu sana na inatukumbusha wajibu wetu wafanyakazi wa kujadiliana kwa pamoja changamoto zilizopo katika utendaji wetu wa kazi na kuzitafutia ufumbuzi kwa pamoja na hatimaye kuleta tija katika maeneo ya kazi”.
Aidha, Mheshimiwa Majaliwa amewapongeza watumishi wote kwa kazi kubwa wanayoifanya katika kuwaletea Watanzania maendeleo. “Sisi sote ni mashahidi wa mafanikio makubwa yaliyopatikana katika kipindi cha miaka mitatu kiuchumi, kisiasa, kidiplomasia na kijamii”
Kaulimbiu ya maadhimisho hayo ni “Nyongeza ya Mishahara ni Msingi wa Mafao Bora na Kinga Dhidi ya Hali Ngumu ya Maisha”