Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Blogu ya Idara ya Habari - MAELEZO

SHIMIWI Kufanyika Iringa, Ni Fursa kwa Wananchi Kiuchumi
Sep 11, 2023
SHIMIWI Kufanyika Iringa, Ni Fursa kwa Wananchi Kiuchumi
Katibu Mkuu Wizara ya Utamaduni, Sanaa na Michezo, Bw. Saidi Yakubu akifanya mazungumzo na Katibu wa Shirikisho la Michezo ya Wizara na Idara za Serikali (SHIMIWI), Bw. Alex Temba leo Septemba 11, 2023 katika ofisi ndogo ya Wizara hiyo jijini Dar es salaam ambapo wamejadili namna bora ya kufanikisha mashindano hayo.
Na Eleuteri Mangi, WUSM, Dar es Salaam

Katibu Mkuu Wizara ya Utamaduni, Sanaa na Michezo, Bw. Saidi Yakubu amekutana na kufanya mazungumzo na Katibu wa Shirikisho la Michezo ya Wizara na Idara za Serikali (SHIMIWI), Bw. Alex Temba ambapo wamejadili namna bora ya kufanikisha mashindano hayo.

Mazungumzo ya Viongozi hao yamefanyika Septemba 11, 2023 katika ofisi ndogo ya Wizara hiyo jijini Dar es salaam kwa lengo la kufanikisha mashindano hayo yanayotarajiwa kufanyika mkoani Iringa kuanzia Septemba 29 hadi Oktoba 14, 2023 ambayo pia yanatoa fursa za kiuchumi kwa wananchi wa mkoa huo.

 

“Wizara yetu ni mlezi wa mashindano haya, taasisi yetu ya Baraza la Michezo la Taifa (BMT) ndiyo Msajili wa SHIMIWI, tupo mstari wa mbele kuunga mkono juhudi za Mhe. Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kuhakikisha watumishi wanafanya mazoezi na kushiriki michezo ili kuboresha afya zao hatua inayosaidia kuboresha utendaji na tija mahala pa kazi”, amesema Katibu Mkuu Bw. Yakubu.

 

Baraza la Michezo la Taifa (BMT) ndiye mlezi wa mashirikisho na vyama vya michezo nchini ikiwemo Shirikisho la Michezo ya Wizara na Idara za Serikali.

 

Kwa upande wake Katibu wa Shirikisho la Michezo ya Wizara na Idara za Serikali (SHIMIWI), Bw. Alex Temba amesema shirikisho hilo linaendelea na maandalizi kulingana na ratiba ya mashindano hayo ilivyopangwa na kuwasisitiza wakazi wa Iringa kujiandaa kupokea ugeni huo ambao utakuwa na manufaa kwa uchumi wa wakazi hao.

 

Mashindano ya SHIMIWI yatahusisha michezo ya mpira wa miguu, netiboli, mchezo wa kuvuta kamba, baiskeli, riadha na michezo ya jadi ambayo inajumuisha mchezo wa vishale, draft, karata na bao.

Mipangilio
Marekebisho ya Mandhari
Marekebisho ya Maandishi