Waziri wa Nishati, Mhe. January Makamba ameeleza kuwa, Serikali imetenga kiasi cha Shilingi bilioni 38 kwa ajili ya ujenzi wa kituo cha kupoza umeme wilayani Urambo Mkoa wa Tabora pamoja na njia ya kusafirisha umeme ya kV 132 kutoka Tabora hadi wilayani humo ili kuifanya wilaya hiyo kuwa na umeme wa uhakika na unaotosheleza mahitaji.
Waziri wa Nishati, alisema hayo tarehe 23 Julai, 2022 baada ya kufika katika Kijiji cha Uhuru wilayani Urambo, ili kukagua kazi za awali zinazoendelea katika eneo lililotengwa kwa ajili ya ujenzi wa kituo cha kupoza umeme.
“Mkoa wa Tabora ulipata umeme miaka ya 1980 baada ya kujenga kituo cha Ibadakuli mkoani Shinyanga lakini watu wanaongezeka, shughuli zinaongezeka na umeme sasa hautoshelezi mahitaji mapya. Urambo pia ilikuwa ikipata umeme huo kwa umbali mrefu hali iliyofanya umeme kuja ukiwa mdogo na unaokatika mara kwa mara.” Alisema Makamba.
Alieleza kuwa, hatua za awali zilizochukuliwa na Serikali ili kurekebisha hali hiyo ni pamoja na kufupisha urefu wa nyaya ili likitokea tatizo popote lisiathiri eneo kubwa na pia kuongeza unene wa nyaya hadi kufikia milimita 100 toka milimita 25 ambapo Shilingi milioni 509 zilitumika kwa kazi ya ubadilishaji wa nyaya hizo kwa urefu wa kilometa 54. Hatua hizo za awali zimewezesha hali ya umeme kuimarika tofauti na hapo awali.
Aliongeza kuwa, hatua za kudumu zinazochukuliwa na Serikali ni kujenga kituo cha kupoza umeme cha Uhuru ambacho kitatoa umeme wa uhakika wilayani humo na kwamba ujenzi wa mradi huo utaanza kutekelezwa mwezi Agosti 2022 na kukamilika mwaka 2023.
Kuhusu fidia ya wananchi waliotoa maeneo ili kutekeleza mradi huo alisema kwamba, fedha zimeshatengwa kiasi cha Shilingi bilioni 4.3 ili kulipa fidia wananchi hao na kwamba malipo yataanza kufanyika baada ya siku 25.
Katika hatua nyingine, Waziri wa Nishati, January Makamba amesisitiza kuwa, Serikali haitaacha kuhamasisha matumizi ya nishati safi ya kupikia kwani ni takwa la Sera ya Nishati ya mwaka 2015 ambayo inaeleza kuwa, Serikali itahakikisha kila Mtanzania anapata nishati safi na salama ya kupikia ambayo anaweza kuhimili bei yake.
“Kama Wizara tumeamua tutoe msukumo mkubwa kwenye nishati safi ya kupikia, mwisho wa mwaka huu tutatengeneza mpango mkakati mkubwa wa kitaifa wa kuanza safari ya kuwawezesha watanzania, hasa kina mama vijijini kuondokana na adha kubwa na hatari kwa afya zao kutokana na kupika kwa kutumia kuni na mkaa.” Alisema Makamba
Aliongeza kuwa, “Watu 22 elfu wanakufa kwa mwaka kutokana na mfumo wa hewa kuathirika kwa sababu ya moshi ambao una sumu, suala hili tumeamua kulibeba kwa nguvu kubwa ili watanzania wote hasa kina mama, maisha yao yawe bora zaidi.”
Mkuu wa Mkoa wa Tabora, Dkt. Balozi Batilda Buriani alipongeza Wizara ya Nishati kwa kuanza kutekeleza mradi huo wa uhamasishaji wa nishati safi ya kupikia na kueleza kuwa suala hilo litapelekea kina mama kuondokana na adha ya moshi na pia kupunguza ukataji wa miti kwa ajili ya utengenezaji wa mkaa.
Akiwa mkoani Tabora, Waziri Makamba pia alifika katika kata ya Ifucha katika Manispaa ya Tabora na wananchi wa eneo hilo walimweleza kuhusu kero ya kutokuwa na umeme ambapo Waziri wa Nishati aliwaahidi kuwa kazi ya kupeleka umeme kwenye Kata hiyo itaanza tarehe 25 Agosti, 2022 na Mkandarasi ameshapatikana ambaye ni kampuni ya Ceylex.
Waziri Makamba anaendelea na ziara katika mikoa mbalimbali nchini akiwa na malengo ya kusikiliza maoni, kero za wananchi na kuzitatua, kukagua miradi ya nishati pamoja na kuhamasisha matumizi ya nishati safi na salama ya kupikia.