Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Blogu ya Idara ya Habari - MAELEZO

Sheria ya Manunuzi Kutambua Makandarasi wa Ndani
Dec 07, 2023
Sheria ya Manunuzi Kutambua Makandarasi wa Ndani
Naibu Waziri wa Ujenzi, Mhandisi Godfrey Kasekenya akizungumza jambo katika hafla ya ugawaji wa Tuzo za Ujenzi na Majengo Afrika Mashariki kwa Mwaka 2023 (EABC), hafla iliyofanyika katika Ukumbi wa Mlimani City, jijini Dar es Salaam.
Na Mwandishi Wetu

Naibu Waziri wa Ujenzi, Mhandisi Godfrey Kasekenya, amesema Serikali itaendelea kuwaamini Wakandarasi wa Ndani kwa miradi mbalimbali ikiwemo ile mikubwa ambayo wanaweza wakafanya vizuri kwani Serikali tayari imeongeza wigo mpana katika sheria ya manunuzi kwa lengo la kuwanufaisha Wazawa.

 

Hayo ameyasema wakati wa Ugawaji wa Tuzo za Ujenzi na Majengo Afrika Mashariki kwa Mwaka 2023 (EABC) zilizofanyika Katika Ukumbi wa Mlimani City jijini Dar es Salaam.

 

Mhandisi Kasekenya amesema Wahandisi wanapaswa wapate vifaa bora ikiwemo saruji, nondo, misumari, vigae, marumaru na bidhaa zote zinazotumika kwenye ujenzi ambazo zinazalishwa na kampuni hizo.

"Ukiwa Mhandisi mzuri halafu ukapata bidhaa zisizo bora basi hautafanya chochote kizuri. Moja ya kitu ambacho Serikali tunakitaka ni kuwa na vifaa na uhandisi bora hivyo tunatoa wito kwa wadau wanaojihusisha eneo hili kutoa huduma zilizo bora ambazo zinaingia kwenye mnyororo mzima wa ujenzi", amesema Mhandisi Kasekenya

 

Hata hivyo Mhandisi Kasekenya ametoa rai kwa Watanzania kuzidi kuwatumia wataalamu wa ujenzi pindi wanapokuwa na miradi ili kuwa na uhakika na usalama wa miradi yao kumalizika kwa wakati na kuwa bora. 

"Usipowatumia wataalamu ujue mbele ya safari inawezekana ukapata hasara. Kama unajenga nyumba hakikisha imesanifiwa na mtaalamu hata asipojenga yeye hakikisha anakupa ushauri”, amesisitiza Naibu Waziri huyo.

 

Tuzo za Ujenzi na Majengo za Afrika Mashariki kwa Mwaka 2023 umeshindanisha makampuni zaidi ya 500 kwa lengo la kuongeza ushindani miongoni mwa wadau wa Sekta ya Ujenzi, lakini pia kufanya chachu ya utoaji wa huduma bora katika mnyororo mzima wa Sekta ya Ujenzi.

 

 

Mipangilio
Marekebisho ya Mandhari
Marekebisho ya Maandishi