[caption id="attachment_52881" align="aligncenter" width="750"] Msajili wa Hazina Bw.Athumani Mbuttuka akizungumza na waandishi wa habari(hawapo pichani) juu ya kuunganishwa kwa benki ya TPB na TIB Corporate leo Jijini Dodoma[/caption]
Na. Immaculate Makilika – MAELEZO
Serikali imeziunganisha benki zake mbili za biashara, Benki ya Posta Tanzania (TPB Bank Plc) na Benki ya Uwekezaji Tanzania (TIB Corporate Limited) ili kuongeza ufanisi na kupunguza gharama za uendeshaji.
Akizungumza leo (Jumatatu Juni 1, 2020) jijini Dodoma, Msajili wa Hazina, Athumani Mbuttuka alisema kuwa Serikali imeendelea kuchukua hatua mbalimbali zenye lengo la kuboresha utendaji wa mashirika na taasisi za umma ikiwemo kuunganisha taasisi zinazotekeleza majukumu yanayofanana, ili kuongeza ufanisi na kupunguza gharama za uendeshaji.
“Kwa muktadha huu, Serikali imeamua kuunganisha benki zake mbili za biashara, yaani Benki ya TPB na Benki ya TIB Corporate kuanzia tarehe 01 Juni 2020. Kwa hatua ya awali, Benki ya TPB itachukua mali na madeni ya Benki ya TIB Corporate na muunganiko huu utafanya benki kuwa na mali takribani trilioni moja”, alisema Mbuttuka
Alifafanua Mbuttuka amesema Serikali imechukua uamuzi huu kwa lengo la kuboresha utendaji wa benki inazozimiliki ili kuwa na benki moja ya biashara ambayo ni imara. Aidha, muungano huu unalenga kuleta mageuzi makubwa ya kiutendajii, kimfumo, kimuundo, na kitaswira ili benki hii iweze kuhimili ushindani wa kibiashara kwenye sekta ya fedha.
“Muunganiko huo hautakuwa na athari katika huduma za kibenki, wala hakuna mfanyakazi atakayepoteza ajira. Aidha, Serikali inapenda kuuhakikishia umma kuwa itaendelea kuhakikisha utendaji wa benki zake unaimarika na maslahi ya wenye amana na wateja wote yanalindwa kwa mujibu wa sheria, kanuni, na taratibu za usimamizi wa benki na taasisi za fedha”, alioneza Mbuttuka.
Kwa mujibu wa Msajili wa Hazina, wateja wote wa Benki ya TPB na Benki ya TIB Corporate wataendelea kuhudumiwa kwenye matawi yao ya sasa hadi hapo watakapotaarifiwa vinginevyo.