Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Blogu ya Idara ya Habari - MAELEZO

Serikali Yazindua Rasmi Ubalozi Algeria
Aug 03, 2023
Serikali Yazindua Rasmi Ubalozi Algeria
Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Dkt. Stergomena Tax akikata utepe kuashiria uzinduzi rasmi wa Ubalozi wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania jijini Algiers, Algeria. Kushoto ni Waziri wa Mambo ya Nje na Diaspora wa Algeria, Mhe. Ahmed Attaf na kulia ni Balozi wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania nchini Algeria, Mhe. Mej. Jen. (Mst), Jacob Kingu wakishuhudia ufunguzi huo.
Na Mwandishi Wetu

Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania imezindua rasmi Ubalozi wake Jijini Algiers, Algeria.
 

Ufunguzi huo umefanywa na Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Dkt. Stergomena Tax na kuhudhuriwa na mwenyeji wake Waziri wa Mambo ya Nje na Diaspora wa Algeria, Mhe. Ahmed Attaf,  Balozi wa kwanza wa Algeria kuhudumu nchini Tanzania, Balozi Noureddine Djoudi na Jumuiya ya Wanadiplomasia nchini Algeria.


Kiwango cha ubadilishaji wa biashara kati ya Tanzania na Algeria ni cha chini ikilinganishwa na fursa nyingi zilizopo. Algeria yenye eneo lake la kimkakati na uchumi inatoa fursa kubwa kwa biashara za Tanzania.

Akihutubia kwenye ufunguzi wa Ubalozi huo, Waziri Tax ameeleza kuwa Tanzania na Algeria zimejidhatiti kuimarisha uhusiano wa kidiplomasia kwa lengo la kukuza ushirikiano wenye maslahi kupitia sekta za kipaumbele kama vile sekta za kilimo, madini, utalii, mafuta na gesi, vifaa tiba, viwanda, nishati pamoja uchumi wa buluu.

Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Dkt. Stergomena Tax akihutubia wakati wa hafla ya ufunguzi wa Ubalozi wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania nchini Algeria.

Ni imani yangu kuwa uzinduzi wa ubalozi huu ni ishara ya kuimarisha ushirikiano kati ya Tanzania na Algeria na kutakuza na kuimarisha ushirikiano wa kiuchumi baina ya mataifa yetu, katika Mkutano wa Tano wa Tume ya Pamoja ya Kudumu ya Ushirikiano kati ya Tanzania na Algeria tulikubaliana kuhusu maeneo ya kipaumbele kwa manufaa ya pande zote mbili na tulisaini Hati nane (8) za Makubaliano ya Ushirikiano katika maeneo ya mafuta na gesi, nishati, elimu, kumbukumbu na nyaraka, uhusiano wa kidiplomasia. Aidha, pamoja na kusainiwa kwa hati hizo za makubaliano, pia tulikubaliana kutoa kipaumbele katika sekta za mafuta na gesi, nishati, kilimo, dawa pamoja na masuala ya amani na usalama", alisema Waziri Dkt. Tax.

Naye Mhe. Attaf ameeleza kuwa ziara ya Waziri Tax imekuwa na mafanikio makubwa kwa kuwa wamepata fursa ya kuzungumza masuala ya ushirikiano katika sekta za biashara, uwekezaji na sekta nyingine muhimu kwa maendeleo ya mataifa hayo mawili.

“Balozi zinafaa kuendelea kuwa madaraja ya muhimu kati ya watu, nchi na mataifa.  Balozi zetu zinawajibika kukuza, kuimarisha ushirikiano na mahusiano kati ya nchi na nchi ili kuleta tija zaidi na kuziwezesha nchi zetu kunufaika kiuchumi’’, amesema Mhe. Attaf

Ufunguzi wa Ubalozi umefanyika pembezoni mwa Mkutano wa Tano wa Tume ya Pamoja ya Kudumu ya Ushirikiano (JPC) kati ya Tanzania na Algeria ambao umemalizika kwa mafanikio na kuwezesha kusainiwa kwa Hati 8 za Makubaliano ya Ushirikiano katika sekta za nishati, mafuta na gesi, elimu na teknolojia, mafunzo ya diplomasia, kumbukumbu na nyaraka, ulinzi na usalama, ushirikiano wa kidiplomasia, kilimo na afya.


Uhusiano kati ya Algeria na Tanzania uliasisiwa mwaka 1963 mara baada ya Uhuru wa Tanganyika. Tangu wakati huo nchi hizi zimeendelea kushirikiana katika maeneo mbalimbali kwa maslahi ya pande zote. Vilevile, katika kuimarisha ushirikiano huo Tanzania imefanya ufunguzi wa Ubalozi wake nchini Algeria ambao ulianza kutekeleza majukumu yake tangu mwaka 2017.


Viongozi wengine waliohudhuria ufunguzi huo ni Katibu Mkuu Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Dkt. Samwel Shelukindo, Katibu Mkuu Wizara ya Afya, Dkt. Seif Shekalaghe, Naibu Makatibu Wakuu kutoka Wizara za Elimu, Sayansi na Teknolojia, Nishati na Mambo ya Ndani ya Nchi.

Mipangilio
Marekebisho ya Mandhari
Marekebisho ya Maandishi