Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Blogu ya Idara ya Habari - MAELEZO

Serikali Yazindua Mwongozo wa Kitaifa wa Uanzishaji na Uendeshaji Majukwaa ya Uwezeshaji Wanawake Kiuchumi
Sep 12, 2022
Na Jacquiline Mrisho

Na Mwandishi Wetu, WMJJWM, Pwani

Serikali imezindua Mwongozo wa Kitaifa wa Uanzishaji na Uendeshaji Majukwaa ya Uwezeshaji Wanawake Kiuchumi wenye lengo la kuleta ufanisi wa utekelezaji wa majukwaa haya ikiwa ni pamoja na kuyafanya yajulikane ngazi zote hapa nchini.

Akizungumza katika uzinduzi wa Mwongozo huo kwa niaba ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Samia Suluhu Hassan, Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum, Mhe. Dkt. Dorothy Gwajima ameitaka jamii kuelimisha wanawake waone umuhimu wa kujiunga na majukwaa ya uwezeshaji wanawake kiuchumi kuanzia ngazi ya kijiji/Mtaa, Kata, Wilaya hadi Taifa ili yawawezeshe kupata sehemu ya kujadili mambo yao kuhusu ujasiriamali na biashara kwa ujumla.

Pia, amezitaka Halmashauri za Wilaya/Manispaa na Majiji ziendelee kutenga fedha za ndani ili kuwawezesha Wanawake, Vijana na Watu wenye ulemavu kukopa na hatimaye kuweza kujiendeleza kiuchumi.

Ametoa rai kwa wanufaika wa mikopo ya asilimia 10 na mikopo ya Maendeleo ya Wanawake (WDF) inayotolewa na Wizara wahakikishe wanarejesha mikopo hiyo kwa wakati ili iwezeshe kuwanufaisha wengine kupata mikopo mapema.

Vilevile, Waziri Dkt. Gwajima ameitaka jamii kutoa fursa sawa kwa wanawake na wanaume kushiriki nafasi za uongozi na maamuzi katika ngazi ya jamii na kuwa sehemu ya maamuzi kwa ustawi wa jamii na Taifa letu.

"Wanawake na wanaume tuzidi kuungana kupinga ukatili wa kijinsia na kwa watoto kwa kusimamia kurithisha misingi ya maadili mema kwa vizazi vyetu kwani ukatili ni adui wa maendeleo ya kiuchumi." alisema Waziri Dkt Gwajima

Akizungumza kwa niaba ya Mkuu wa Mkoa wa Pwani, Mkuu wa Wilaya ya Kibaha, Mhe. Sarah Msafiri amesema kuwa kupitia Mwongozo huo Mkoa wa Pwani kupitia Mwongozo huo imeanzisha Kampuni ya Go Mama PLC inayofanya shughuli zake mkoani humo ili kuunganisha wanawake wote kutekeleza shughuli mbalimbali za uwezeshaji wanawake kiuchumi.

Akieleza kuhusu Mwongozo huu, Katibu Mkuu wa Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum, Dkt. Zainab Chaula amesema Wizara iliona umuhimu wa kuwa na Mwongozo huu ili kuwa na ufanisi katika ushiriki wao kwenye shughuli za maendeleo zitakazosaidia kuwakwamua kiuchumi.

Akitoa salamu za Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto kutoka Serikali ya Mapinduzi Zanzibar, Katibu Mkuu wa Wizara hiyo, Mariam Juma Abdallah amesema Wizara hiyo itasimamia utekelezaji wa Mwongozo huo ili kuwawezesha Wanawake hasa wajasiriamali kujikwamua kiuchumi kupitia shughuli zao mbalimbali.

Naye Mwenyekiti wa Chama cha Wanawake Wafanyabiashara (TWCC), Mwajuma Hamza amesema Chama hicho kimefarijika kuona kuwa Serikali imejipanga katika kuhakikisha inawezesha Wanawake hasa katika kuwakwamua kiuchumi kwa kuweka Mwongozo utakaosaidia kuratibu uanzishaji na uendeshaji wa Majukwaa hayo.

Akizungumza katika uzinduzi wa Mwongozo huo, Katibu Mtendaji wa Baraza la Uwezeshaji Wananchi Kiuchumi, Bein'g Issa amesema Baraza lao limeweka mikakati mbalimbali ya kuwezesha wanawake kiuchumi kwa kushirikiana na Wizara ambapo waliratibu uanzishaji wa Majukwaa hayo katika ngazi za Vijiji/ Mitaa, Kata, Wilaya na Mkoa.

Ameongeza kuwa uanzishaji wa Majukwaa umesaidia kutoa elimu ya ujasiriamali kwa wanawake wajasirimali na jumla ya Majukwaa 26 yameanzishwa katika mikao ya Tanzania Bara, Majukwaa 151 katika Halmashauri, Majukwaa 1,354 ngazi ya Kata na Majukwaa 1,859 katika ngazi ya vijijini/ Mitaa.

"Katika haya yote Mikoa mingi imefanya ubunifu ikiwemo kuanzisha makampuni, vikundi vya wajasirimali ambapo imesaidia kuwawezesha kiuchumi Wanawake hasa wajasirimali" alisema Bi. Issa

Mwenyekiti wa Wafanyabiashara Wanawake Mkoa wa Pwani, Mariam Ulega ameishukuru Serikali kwa jitihada zake katika kuhakikisha inaweka mifumo mizuri katika kuwawezesha Wanawake hasa wajasirimali katika kupata fursa za kuanzisha biashara na kupata masoko ya bidhaa zao kwa ustawi na maendeleo ya familia na taifa.

Mipangilio
Marekebisho ya Mandhari
Marekebisho ya Maandishi