Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Blogu ya Idara ya Habari - MAELEZO

Serikali Yaweka Mikakati Kukabiliana na Ukatili wa Kijinsia
Sep 18, 2023
Serikali Yaweka Mikakati Kukabiliana na Ukatili wa Kijinsia
Mkurugenzi wa Idara ya Habari-MAELEZO na Msemaji Mkuu wa Serikali, Bw. Gerson Msigwa akizungumza katika Mkutano wa Wabunge na Wadau wa Sekta ya Habari uliohusu kukabiliana na ukatili wa kijinsia kupitia mitandao ya kijamii uliofanyika leo Septemba 18, 2023 jijini Dar es Salaam.
Na Grace Semfuko - MAELEZO

Msemaji Mkuu wa Serikali na Mkurugenzi wa Idara ya Habari-MAELEZO, Bw. Gerson Msigwa amesema Serikali imeweka mikakati ya kukabiliana na ukatili wa kijinsia hususan kwa wanawake kwenye maeneo mbalimbali nchini, ikiwepo kuanzisha Wizara ya Maendeo ya Jamii, Jinsia, wanawake na Makundi Maalum ambayo imekuwa kinara kushughulikia changamoto hizo.

Amesema ukatili dhidi ya wanawake ni jambo ambalo halikubaliki mahali popote ikiwepo kwenye vyumba vya habari, hivyo Serikali inashirikiana na wadau mbalimbali, kuhakikisha kunakuwa na kampeni za kukabiliana  na hali hiyo hususan kwenye mitandao ya kijamii ambako kumekuwa na udhalilishaji wa kundi hilo.

Aliyasema hayo leo Septemba 18, 2023 katika Mkutano wa Wabunge na Wadau wa Sekta ya Habari uliohusu kukabiliana na ukatili wa kijinsia kupitia mitandao ya kijamii na hasa wanawake, ambao umefadhiliwa na Shirika la Umoja wa Mataifa la Elimu, Sayansi na Utamaduni- UNESCO uliofanyika Jijini Dar es Salaam.

“Ukatili dhidi ya wanawake iwe kwenye vyombo vya habari, kwenye jamii na mahali pengine popote haukubaliki. Serikali imekuwa ikishirikiana na wadau kuhakikisha kwamba kunakuwa na kampeni mbalimbali za kukabiliana na ukatili dhidi ya wanawake, na sasa hivi kumeanza kuja kwa kasi sana ukatili unaofanywa dhidi ya wanawake kwenye mitandao ya kijamii, kwenye majukwaa ya mitandaoni, hili ni jambo ambalo halikubaliki,” amesema Bw. Msigwa.

Kuhusu ukatili wa wanawake kwenye vyombo vya Habari, Bw. Msigwa anasema Serikali inakamilisha kanuni zitakazoleta usawa wa kijinsia kwenye vyombo hivyo.

“Kwa upande wa vyombo vya habari, tunayo sheria yetu ya huduma za habari ambayo tumeifanyia marekebisho hivi karibuni, na sasa waziri anakamilisha kanuni, kwenye zile kanuni moja ya maeneo ambayo tunakwenda kuangalia ni namna gani ambavyo tutaongeza idadi ya wanawake kwenye vyombo vya habari, kwenye vyumba vya uhariri, wawepo wa kutosha, lakini pia tunakwenda kuangalia ni namna gani kanuni zetu zimechukua hatua dhidi ya vitendo hivyo ambavyo pia kwenye vyombo vya habari vinajitokeza,” amesema Bw. Msigwa.

Kwa upande wake Mbunge wa Viti Maalum, Mhe. Neema Lugangira amesema ni lazima jamii na watumiaji wa mitandao wajengewe uelewa ili kuepukana na ukatili huo pamoja na kuwa na sheria ambazo zinalinda kila mtu kuweza kushiriki katika mitandao kwa usawa.

Ni lazima tufanye kampeni ya kitaifa, ni lazima tujenge uelewa wa wadau, watumiaji wa mitandao ya kijamii lakini pia kuweka sheria ambazo zinalinda kila mtu kuweza kushiriki katika mitandao kwa usawa, na tumeshaambiwa kwamba Serikali italeta Bungeni Sheria ya vyama vya siasa na sheria ya uchaguzi, kwa hiyo na sisi tujitajipange kuchangia ipasavyo katika maeneo hayo ili sheria hizo pia zitambue ukatili wa jinsia katika mitandaio ya kijamii,” amesema Mhe. Lugangira.

Mipangilio
Marekebisho ya Mandhari
Marekebisho ya Maandishi