Na Immaculate Makilika – MAELEZO
Serikali imeeleza kuwa haina malengo ya kutoza wananchi wake kodi au tozo kwa ajili ya kuwapa mzigo tu, bali inalenga kuwahusisha Watanzania wote kwa umoja wao katika juhudi za kujikwamua kimaendeleo.
Akitoa kauli ya Serikali kuhusu tozo leo Bungeni jijini Dodoma, Waziri wa Fedha na Mipango, Mhe. Dkt. Mwigulu Nchemba ameeleza kuwa, makusanyo ya tozo ya miamala yameiwezesha Serikali kutoa huduma za msingi kwa wananchi ambapo katika mwaka wa fedha 2021/22, Serikali ilitumia jumla ya Shilingi bilioni saba zilizotokana na tozo ya miamala kwa ajili kujenga madarasa.
Vilevile, Serikali ilitumia jumla ya Shilingi bilioni 143.7 kwa ajili ya ujenzi wa vituo vya afya ambapo kati ya fedha hizo, Shilingi bilioni 117 sawa na asilimia 81.4 ya fedha zote zilitokana na tozo ya miamala. Aidha, Serikali ilitumia jumla ya Shilingi bilioni 611.3 kwa ajili ya mikopo ya Elimu ya Juu na kati ya fedha hizo, Shilingi bilioni 221.3 zilitokana na tozo.
Licha ya kuwa Serikali imetekeleza miradi hiyo kwa ajili ya kusogeza huduma mbalimbali kwa Watanzania, pia imekuwa radhi kufanya marekebisho ya miamala ya kielektroniki iliyolalamikiwa na wananchi.
Waziri Mwigulu anasema “Kufuatia malalamiko hayo, Kamati Kuu ya Chama Cha Mapinduzi chini ya Mwenyekiti wake Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan, iliielekeza Serikali kupitia upya tozo za miamala na kuzingatia maoni ya wananchi”.
Anasisitiza kuwa “Wizara ya Fedha na Mipango kupitia wataalam wake wa Bajeti na wataalam wa Sera huku wakiwashirikisha wadau, wamefanyia kazi maelekezo ya Chama na ya Mhe. Rais Samia Suluhu Hassan kwa kupitia upya tozo hizo”.
Waziri Mwigulu ametaja marekebisho yatakayoanza kutumika Oktoba 1 mwaka huu kuwa ni kufuta tozo ya kuhamisha fedha kutoka benki kwenda mitandao ya simu (pande zote), kufuta tozo ya kuhamisha fedha ndani ya benki moja (pande zote), kufuta tozo ya kuhamisha fedha kutoka benki moja kwenda benki nyingine (pande zote) na Wafanyabiashara (merchants) hawatahusishwa kama ilivyo kwenye kanuni za sasa.
Aidha, marekebisho mengine yaliyofanywa na Serikali ni kusamehe tozo ya miamala kwenye utoaji wa fedha taslimu kupitia wakala wa benki na ATM kwa miamala yenye thamani isiyozidi Shilingi 30,000 na kupunguza gharama ya miamala kwa asilimia 10 hadi asilimia 50 kufuatana na kundi la miamala.
Ikumbukwe kuwa viwango vya tozo vilishushwa kwa asilimia 30 kutoka kiwango cha juu cha Shilingi 10,000 hadi kiwango cha juu cha Shilingi 7,000, viwango ambavyo vilianza kutumika tarehe 07 Septemba, 2021. Kadhalika, Mheshimiwa Rais alisisitiza kupunguzwa zaidi tozo ambapo Wizara ya Fedha ilipunguza tozo zaidi kwa kushusha tena kiwango cha juu kutoka 7,000 hadi 4,000.
Sambamba na hatua hiyo, Serikali inafuta utaratibu wa kodi ya zuio inayotokana na pango kukusanywa na mpangaji na badala yake jukumu hilo linarejeshwa kwa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) kwa utaratibu utakao bainishwa kwenye kanuni.
Mwisho