Na WMJJWM, Dodoma
Serikali kupitia Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maaalum imewapongeza Wabunge kwa utayari wao na kuwa mstari wa mbele katika suala la Elimu ya Malezi, Makuzi na Maendeleo ya Awali ya Mtoto.
Akifungua Semina kwa Wabunge kwa niaba ya Waziri wa Maendeleo ya jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Novemba 09,2022, Naibu Waziri wa Wizara hiyo, Mwanaid Ali Khamis amesema kujitokeza kwa zaidi ya Wabunge 70 ni ishara kwamba wawakilishi hao wa wananchi wameonesha utayari katika suala la kusaidia kusukuma mbele ajenda ya elimu hii kwa wananchi.
“Waheshimiwa Wabunge kutoka Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Huduma na Maendeleo ya Jamii, Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Bajeti na Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Utawala na Serikali za Mitaa tunawashukuru kwa utayari wenu wa kushiriki katika mafunzo haya muhimu”, alisema Mwanaid.
Kwa upande wake Katibu Mkuu wa Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum, Dkt. Zainab Chaula, amewaambia wawakilishi hao wa wananchi kuwa, kundi hilo ni muhimu kwani wao ndio wawakilishi wa wananchi hivyo kuwapatia mafunzo ni mwanzo mzuri wa kuweza kufikisha elimu kwa jamii.
Dkt. Chaula amesema kuwa tangu mwaka 1998, Serikali ilitengeneza Sera ya Mtoto lakini pia Mwaka 2009 ikatunga Sheria ya Mtoto sambamba na marekebisho yake ya 2019 vyote hivyo ni jitihada za kuonesha kuwa Serikali inawajali watoto wa taifa hili.
“Pamoja na kuwa na Sera na Sheria, lakini tukaona ni vema sasa ili hivi viweze kuwa na mashiko, ni kuwapatia elimu wawakilishi wa wananchi na ndio maana mnaona leo tupo hapa, kwani hii itasadia kuleta chachu ya Malezi”, alisema Dkt. Chaula.
Naye Makamu Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Huduma na Maendeleo ya Jamii, Mhe. Aloyce Kamamba, akiongea kwa niaba ya Wabunge wa kamati zote ameipongeza Wizara kwa jitihada inazochukua na kazi wanayoifanya huku akiwataka Wabunge hao kuipeleka elimu hiyo kwa wabunge wenzao lakini pia wananchi wa majimbo yao.
“Waheshiwa Wabunge kwa ‘dose’ hii ambayo tumeipata, tuipeleke kwenye majimbo yetu lakini tuiombe Wizara, iweze kuifikisha elimu hii kwa wabunge wote, leo sisi tumekuja tukiwa zaidi ya watu 78 lakini wapo wenzetu wengine, hivyo itakuwa vizuri na wao wakapata elimu hii”, alisema Kamamba.
Awali akitoa wasilisho kuhusu Malezi ya Awali ya mtoto, Bw Frank Samson alisema katika hatua za ukuaji wa Mtoto imethibitika kuwa umri kati ya miaka 0 hadi 08 ndio kipindi ambacho ubongo wa mtoto hukua kwa asilimia 80, hivyo akawaomba wabunge hao kuzingatia zaidi umri huo kwao wenyewe na kwa wananchi kwenye hatua za awali za Makuzi ya Mtoto.