Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Blogu ya Idara ya Habari - MAELEZO

Serikali Yawahakikishia Ushirikiano Wawekezaji Sekta ya Mifugo
Oct 13, 2022
Na Jacquiline Mrisho


Na Mbaraka Kambona

Katibu Mkuu, Wizara ya Mifugo na Uvuvi (Mifugo), Bw. Tixon Nzunda amesema kuwa Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Rais, Mhe.  Samia Suluhu Hassan inaunga mkono uwekezaji unaofanywa katika sekta ya mifugo hapa nchini, hivyo wataendelea kuwapa ushirikiano wawekezaji hao ili kuhakikisha malengo ya uwekezaji wao yanafikiwa kama walivyotarajia.

Nzunda alitoa kauli hiyo wakati wa ziara yake aliyoifanya mkoani Pwani na Dar es Salaam Oktoba 12, 2022.

Akiwa katika ziara hiyo ambapo alitembelea kiwanda cha kuzalisha chanjo za mifugo cha HESTER, kiwanda cha kuchakata nyama cha TANCHOICE na kampuni ya kuzalisha hereni za kielekroniki za mifugo ambapo kwa nyakati tofauti aliwashukuru Wawekezaji hao kwa sababu uwekezaji wao unaenda sambamba na mipango ya Serikali ya kukuza na kuimarisha sekta ya mifugo nchini.

"Tunawashukuru kwa kuendelea kuunga mkono juhudi za Serikali hususan katika kuimarisha mpango wa mabadiliko wa sekta ya mifugo na tutaendelea kufanya kazi kwa pamoja ili sekta hii iweze kukua zaidi", alisema.

Aliongeza kwa kusema kuwa, Serikali itaendelea kutatua changamoto zinazosababisha kukwamisha uwekezaji ikiwemo mlolongo wa tozo ili kuendelea kujenga mazingira bora ya uwekezaji nchini.

Naye, Mtendaji Mkuu, Kiwanda cha Kuzalisha chanjo za mifugo cha HESTER, Dkt. Furaha Mramba alisema anamshukuru Rais Samia kwa kuweka mazingira mazuri ya uwekezaji huku akiongeza kuwa kiwanda hicho kitaleta faida kubwa nchini ikiwemo fedha za kigeni kupitia uuzaji wa chanjo za mifugo nje ya nchi.

Mkurugenzi Mkuu wa Kiwanda cha TANCHOICE, Bw. Rashid Abdillahi aliiomba Serikali iangalia utaratibu wa usafirishaji wa mifugo nchini hususan katika mizani kwa sababu kwa sasa unasababisha gharama za uendeshaji wa biashara ya nyama kuwa kubwa.

Aidha, katika ziara hiyo, Katibu Mkuu Nzunda alieleza pia namna ambavyo Serikali imejipanga kuanzia mwaka huu wa fedha kuleta mabadiliko katika sekta ya mifugo ikiwemo kuboresha shughuli za ugani, kujenga majosho, minada na kuifufua NARCO pamoja na mashamba mengine ya Serikali.

Mipangilio
Marekebisho ya Mandhari
Marekebisho ya Maandishi