Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Blogu ya Idara ya Habari - MAELEZO

Serikali Yavutia Wawekezaji Sekta ya Nishati
May 31, 2018
Na Msemaji Mkuu

Na Mwandishi wetu

SERIKALI imewataka wawekezaji wa ndani na nje ya nchi kuwekeza katika miradi ya ujenzi wa viwanda nchni kwa kuwa Tanzania imejipanga katika kuzalisha kiasi kikubwa cha nishati ya umeme nchini kupitia miradi mbalimbali ya kimkakati.

Hayo yamesemwa mwishoni mwa wiki Mkoani Kilimanjaro na Mkurugenzi wa Idara ya Habari (MAELEZO) na Msemaji Mkuu wa Serikali, Dkt. Hassan Abbasi wakati wa mahojiano ya kipindi maalum cha Redio ya Sauti ya Injili FM, akielezea kuhusu utekelezaji wa sera, program, miradi ya mageuzi ya kiuchumi inayotekelezwa katika Serikali ya Awamu ya Tano.

Dkt. Abbasi alisema sera ya uchumi wa viwanda ni ajenda kuu ya kimkakati iliyopewa msisitizo katika Serikali ya Awamu ya Tano ikilenga katika kufanya mageuzi ya kiuchumi katika sekta kuu za kiuchumi ikiwemo kilimo, hatua inayolenga kuongeza wigo mpana wa ajira kwa Watanzania walio wengi zaidi.

“Ili kuweza kuwa na viwanda vya kisasa, Serikali imefanyafanya mageuzi makubwa katika eneo la uzalishaji wa umeme, ipo miradi mikubwa minne ya kitaifa  ikiwemo mradi wa umeme wa gesi wa kinyerezi, mradi wa kwanza wa megawati 150 umekamilika na sasa tunaendelea na upanuzi ili kuzalisha megawati 180” alisema Dkt. Abbasi.

Aidha Dkt. Abbasi alisema uzalishaji wa ongezeko la ziada la umeme huo wa gesi wa megawati 180 katika mradi wa Kinyerezi I utasaidia katika upatikanaji wa umeme katika mikoa mingi zaidi nchini, sambamba na upatikanaji wa megawati 240 uliopo sasa katika mradi wa kinyerezi II ambao hadi kufikia mwishoni mwa mwaka huu utaweza kuzalisha kiasi hicho cha umeme.

Akifafanua zaidi, Dkt. Abbasi alisema Serikali ya Awamu ya Tano pia mbioni kutekeleza mradi wa kihistoria kuzalisha umeme kwa kutumia maji wa Stieglers Gorge wenye uwezo wa kuzalisha Megawati 2100, ambapo katika kipindi cha miaka 3 ijayo Serikali itaweza kuzalisha Megawati mpya 4000 katika miradi mbalimbali inayoendelea kujengwa nchini.

Kwa mujibu wa Dkt. Abbasi alisema Serikali pia inatekeleza mradi mkubwa wa kujenga nguzo kubwa za kisasa wa ‘Backborne Project’ kwa ajili ya kusafirisha umeme katika mikoa yote nchini, unaolenga kubadilisha mifumo ya zamani ya njia ya kusafirisha umeme ikiwemo.

Alisema malengo ya Serikali ni kuhakikisha kuwa kupitia miradi hiyo mikubwa ya umeme, dhana ya uchumi wa viwanda inaweza kuleta matokeo chanya kwa wananchi wake kuweza kuajiriwa na kuondoa changamoto ya ajira kwa vijana wengi nchini.

“Katika kituo cha uwekezaji tumeweka mazingira ya unafuu kwa wawekezaji kupata unafuu wa kodi wa kuagiza vifaa pamoja na kutenga maeneo maalum ya uwekezaji na kusogeza huduma muhimu kwa wawekezaji ikiwemo umeme na maji” alisema Dkt. Abbasi.

Dkt. Abbasi anasema kupitia dhana ya uchumi wa Viwanda, Serikali imekusudia kufufua na kujenga viwanda vingi zaidi nchini ikiwemo maboresho ya miundombinu ya viwanda vyote vilikuwepo katika awamu mbalimbali za uongozi.

Aliongeza kuwa katika kuhakikisha kuwa dhamira hiyo ya Serikali ya awamu ya Tano inakamilika, Serikali tayari imetoa maelekezo kwa wadau mbalimbali wa maendeleo pamoja na kuweka msisitizo kwa Viongozi na watendaji mbalimbali wa Serikali ikiwemo Wakuu wa Mikoa.

Mipangilio
Marekebisho ya Mandhari
Marekebisho ya Maandishi