Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Blogu ya Idara ya Habari - MAELEZO

Serikali Yaviagiza Vyuo Vikuu Kuwasajili Wanafunzi Mara Moja
Nov 09, 2017
Na Msemaji Mkuu

Na: Lilian Lundo – Dodoma.

Serikali imeviagiza vyuo vikuu nchini kuacha urasimu katika kuwasajili wanafunzi ambao ni wanufaika wa mikopo ya Elimu ya Juu.

Kauli hiyo imetolewa na Waziri wa Elimu Sayanzi na Teknolojia Prof. Joyce Ndalichako alipokuwa akitoa kauli ya Serikali kuhusu udahili na utoaji wa mikopo kwa wanafunzi wa elimu ya juu kwa mwaka 2017/18, leo Bungeni, Mjini Dodoma.

“Kwa mara nyingine naviagiza vyuo vyote vya Elimu ya Juu nchini, kuondoa urasimu katika kuwasajili wanafunzi vyuoni. Inasikitisha sana kuona kuwa baadhi ya vyuo vinadiriki hata kuwakataa wanafunzi waliowadahili wao wenyewe au vinawalazimisha wachukue program tofauti na walizokuwa wamechaguliwa awali na vyuo husika,” alisema Prof. Ndalichako.

Prof. Ndalichako amesema, jambo hilo halikubaliki hata kidogo na linaleta shaka kuhusu uadilifu wa vyuo husika, hivyo ameiagiza Tume ya Vyuo Vikuu Tanzania (TCU) na Kurugenzi ya Elimu ya Juu ya Wizara ya Elimu kufuatilia kwa ukaribu mambo yote yanayoendelea vyuoni wakati wanafunzi wanaripoti na kuwabainisha wote wanaokiuka taratibu na kuwanyima wanafunzi haki yao ya kusoma program wanazozitaka.

“Serikali haitasita kuchukua hatua kali, kwa vyuo vyote vitakavyoleta usumbufu usio wa lazima kwa wanafunzi na kuwafanya wapoteze muda ambao wanapaswa kuutumia kwa masomo,” alifafanua Prof. Ndalichako.

Aidha amesema, mikopo inayotolewa kwa wanufaika hao ni makubaliano baina ya wanufaika na Serikali na mwisho wa siku watapaswa kuzirejesha fedha hizo. Hivyo Vyuo vinapaswa kuwasajili wanafunzi wote kwa kuzingatia taratibu zilizopo na mazingira halisi yanayojitokeza.

Prof. Ndalichako amemshukuru Rais Dkt. John Pombe Magufuli kwa uongozi wake uliotukuka kwa kuwajali watanzania wote ikiwa ni pamoja na wanafunzi wa Elimu ya Juu, ambapo haijawahi kutokea fedha kwa ajili ya mikopo ya wanafunzi wa Elimu ya Juu zikatolewa mwezi mzima kabla ya vyuo kufunguliwa.

“Wizara yangu haitakuwa na huruma na Chuo ambacho kitachelewesha malipo kwa wanafunzi wanufaika wa mikopo. Hatuwezi kuruhusu mtu yoyote au chuo chochote kiwe ni cha umma au binafsi, kuhujumu kazi nzuri inayofanywa na Mheshimiwa Rais wetu mpendwa wa Awamu ya Tano,” alifafanua Ndalichako.

Hata hivyo, Bodi ya Mikopo ya Wanafunzi wa Elimu ya Juu inakamilisha utaratibu wa kufungua dirisha la rufaa kwa ajili ya wanafunzi watakaokuwa hawajapangiwa mikopo kufikia Novemba 10 mwaka huu ili kuwawezesha kuwasilisha rufaa zao ili wale watakaofanikiwa kwenye rufaa wapangiwe mikopo kabla ya Novemba 30, mwaka huu.

Vigezo vilivyowekwa katika utoaji wa mikopo ni pamoja na Ulemavu, Uyatima na Uhitaji hasa katika program za kipaumbele ambapo kwa mwaka 2017/18 Serikali kupitia Bodi ya Mikopo ya Wanafunzi wa Elimu ya Juu imepanga kutumia Shilingi Bilioni 427.54 kugharamia mikopo kwa ajili ya wanafunzi wenye uhitaji na waliodahiliwa na Vyuo vya Elimu ya Juu hapa Nchini.

Mipangilio
Marekebisho ya Mandhari
Marekebisho ya Maandishi