Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Blogu ya Idara ya Habari - MAELEZO

Serikali Yaunda Timu Kuishauri Namna ya Kuendeleza Waandishi wa Vitabu Nchini-Waziri Mkenda
Jul 03, 2022
Na Jacquiline Mrisho

Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Mhe. Prof Adolf Mkenda akizungumza na Mwandishi mkongwe wa Riwaya nchini, Ndg Shafi Adam Shafi wakati alipowasili katika ukumbi wa NSSF Ilala Jijini Dar es salaam kwa ajili ya tukio la Elite Mjue Mtunzi lililofanyika tarehe 3 Julai 2022 likiwa na lengo la kutoa Ngao ya Mtunzi kama heshima na kutambua kazi za waandishi iliyotolewa na Umoja wa waandishi wa Riwaya wenye Dira (UWARIDI).

Na Mathias Canal, WEST-Dar es salaam

Serikali imeeleza inao wajibu kuwaenzi waandishi wake kama ambavyo inapaswa kuwaenzi watu wengine wote wanaoweka jitihada za dhati kwa manufaa chanya ya taifa.

Namna ya kwanza ya kuthamini jitihada za waandishi wa vitabu ni kununua na kusoma kazi zao. Kama alivyopata kusema mwandishi nguli wa Afrika Mashariki, hayati Sheikh Shaaban Robert, “Mwandishi si mtu wa ajabu awezaye kuishi kwa kula hewa na kunywa ukungu. Ni mtu wa desturi ambaye, kama watu wengine wa desturi, hafarijiwi na hasara.”

Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Mhe. Prof Adolf Mkenda akimpatia Ngao ya Mtunzi, Bi. Elizabeth Mramba ikiwa ni heshima na kutambua kazi za waandishi wakati iliyotolewa na Umoja wa waandishi wa Riwaya wenye Dira (UWARIDI) wakati aliposhiriki kwenye tukio la Elite Mjue Mtunzi lililofanyika tarehe 3 Julai 2022 katika ukumbi wa NSSF Ilala Jijini Dar es salaam. Kulia ni Rais wa Umoja wa waandishi wa Riwaya wenye Dira (UWARIDI) Ndg Hussein Tuwa.

Hayo yamebainishwa na Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Mhe Prof Adolf Mkenda aliposhiriki kwenye tukio la Elite Mjue Mtunzi lililofanyika tarehe 3 Julai 2023 katika ukumbi wa NSSF Ilala Jijini Dar es salaam ambapo amegawa Ngao ya Mtunzi ikiwa ni heshima na kutambua kazi za waandishi.

Amesema kuwa katika kutambua umuhimu wa waandishi wa vitabu, kwa mwaka huu wa fedha 2022/2023 Serikali imeunda timu inayoongozwa na Profesa Penina Mlama, ambayo itakuwa na jukumu la kuishauri Wizara namna bora ya kuendeleza waandishi wa vitabu nchini.

Waziri Mkenda amesema kuwa Kwa mwaka wa fedha 2022/23 Serikali itaanza kutoa tuzo kwa waandishi bora wa vitabu kwa matumizi ya shule kwa lengo la kutoa hamasa kwa waandishi wa vitabu nchini ili kuongeza upatikanaji wa vitabu kwa ajili ya ufundishaji na ujifunzaji.

Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Mhe. Prof Adolf Mkenda akiwa katika picha ya pamoja na waandishi nguli nchini walioshiriki kwenye tukio la Elite Mjue Mtunzi kwa ajili ya utoaji Ngao ya Mtunzi iliyotolewa na Umoja wa waandishi wa Riwaya wenye Dira (UWARIDI) ikiwa ni heshima na kutambua kazi za waandishi lililofanyika tarehe 3 Julai 2022 katika ukumbi wa NSSF Ilala Jijini Dar es salaam.

Amesema kuwa serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania inayoongozwa na Mhe Rais Samia Suluhu Hassan inafurahi kuona jitihada za Watanzania katika kuikuza lugha la Kiswahili kupitia riwaya kwani ukiachilia mbali kuitangaza vema nchi, pia inapanua wigo wa maarifa na ajira miongoni mwa Watanzania.

Waziri Mkenda ametoa rai kwa waandishi kupitia umoja wa UWARIDI kupeleka mezani mapendekezo na ushauri wa namna gani bora ya kufanikisha zaidi uandishi wa vitabu kwa manufaa siyo tu ya waandishi, bali pia, taifa kwa ujumla.

Waziri Mkenda ameipongeza kampuni ya ELITE BOOKSTORE, kwa kudhamini utoaji Ngao ya Mtunzi ikiwa ni pamoja na uzinduzi wa vitabu kwani huo ni mfano wa kuigwa na makampuni na mashirika mengine pia.

Kadhalika, Waziri Mkenda amesema kuwa Wizara ya Elimu, Sayansi na teknolojia inaalika makampuni na mashirika kushirikiana katika uendelezaji wa waandishi nchini.

“Tukiwa na machapisho mengi na mazuri, tutaweza pia kuendeleza tabia ya watu kupenda kusoma vitabu nchini. Mwisho niwashukuru sana kwa kunialika nawaomba tuendelee kushirikiana katika kuliendeleza taifa letu” Amekaririwa Prof Adolf Mkenda

Kuunga mkono kazi za waandishi wetu kwa kununua nakala hali ni kuwaondolea hasara ambazo kimsingi haziwafariji maishani zaidi ya kuwatia umasikini.

Mipangilio
Marekebisho ya Mandhari
Marekebisho ya Maandishi