Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Blogu ya Idara ya Habari - MAELEZO

Serikali Yaunda Kamati ya Kutatua Migogoro ya Mipaka Kati ya Vijiji na Hifadhi ya Wembere
Dec 06, 2022
Na Jacquiline Mrisho

Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii, Mhe. Mary Masanja (Mb) akizungumza na wananchi kuhusu Serikali kuunda kamati ya kutatua migogoro ya mipaka katika Hifadhi ya Bonde la Wembere kwenye mkutano uliofanyika kijiji cha Ujungu Wilaya ya Iramba mkoani Singida.

Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii, Mhe. Mary Masanja (Mb) amesema Serikali itaunda Kamati ya kuangalia migogoro ya mipaka na vijiji vinavyozunguka Msitu wa Hifadhi wa Bonde la Wembere uliopo katika Halmashauri ya Wilaya ya Iramba mkoani Singida.

Ameyasema hayo leo alipokuwa akizungumza na wananchi kuhusu mgogoro wa mipaka kwenye eneo la ardhioevu katika Kijiji cha Msai na Ujungu mkoani Singida.

Amesema Kamati hiyo itaishauri Serikali endapo kuna umuhimu wa kurekebisha mipaka na kama eneo hilo litafaa kwa ajili ya shughuli za kibinadamu au la.

"Kuanzia leo tunaunda Kamati ambayo itajumuisha wataalam kutoka ngazi ya Wizara, Mkoa na Wilaya na zoezi hilo litaanza mara moja na itapitia mipaka kwa kushirikiana na wananchi ili kuainisha mipaka halisi kwa kuzingatia ramani iliyopo ili kumaliza mgogoro huo", Mhe. Masanja amesisitiza.

Baadhi ya wananchi wakimsikiliza Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii, Mhe. Mary Masanja (Mb) (hayupo pichani) alipokuwa akizungumza kuhusu Serikali kuunda kamati ya kutatua migogoro ya mipaka katika Hifadhi ya Bonde la Wembere kwenye mkutano uliofanyika katika Kijiji cha Ujungu, Wilaya ya Iramba mkoani Singida.
Mbunge wa Iramba Magharibi ambaye pia ni Waziri wa Fedha na Mipango, Mhe. Dkt. Mwigulu Nchemba akiwataka wananchi kutoa ushirikiano wakati wa zoezi la kupima mipaka kati ya vijiji na Hifadhi ya Bonde la Wembere kwenye mkutano uliofanyika kijiji cha Ujungu,Wilaya ya Iramba mkoani Singida.

Mhe. Mary Masanja amewataka wananchi hao kuzingatia sheria za kutovamia maeneo ya hifadhi na kuwa walinzi wa eneo hilo mara tathmini itakapokamilika. 

Kuhusu changamoto ya wafugaji wanaopitisha ng'ombe katikati ya hifadhi kwa ajili ya kupeleka mifugo yao kunywa maji amesema, Serikali itaangalia namna iliyo bora ya kutatua changamoto hiyo ili wananchi wasiingiliane na masuala ya uhifadhi.

Sambamba na hilo amewataka wananchi waache tabia ya kukata miti hovyo na kukubaliana na mradi wa upandaji miti ulioletwa na Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania (TFS) kwa lengo la kukabiliana na mabadiliko ya tabia ya nchi.

Naye, Mbunge wa Iramba Magharibi ambaye pia ni Waziri wa Fedha na Mipango, Mhe. Dkt. Mwigulu Nchemba amewataka viongozi wa Kata na vijiji kushirikiana na Kamati iliyoundwa wakati wa kupitia upya usahihi wa vigingi zilizowekwa.

Mbunge wa Iramba Magharibi ambaye pia ni Waziri wa Fedha na Mipango, Mhe. Dkt. Mwigulu Nchemba (wa pili kulia) akiwa ameongozana na Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii, Mhe. Mary Masanja (Mb) (katikati) na Kamati ya Ulinzi na Usalama ya Wilaya ya Iramba kukagua eneo la kitalu cha miche ya miti la Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania (TFS) lililoharibiwa na wananchi katika Wilaya ya Iramba mkoani Singida.
Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii, Mhe. Mary Masanja (Mb) akiwaasa Watendaji wa Kijiji kuhusu kuelimisha wananchi juu ya umuhimu wa upandaji miti katika kitalu cha miche ya miti cha TFS kilichoharibiwa na wananchi kwenye Hifadhi ya Bonde la Wembere, Wilaya ya Iramba mkoani Singida.

Mipangilio
Marekebisho ya Mandhari
Marekebisho ya Maandishi