Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Blogu ya Idara ya Habari - MAELEZO

Serikali Yatumia Bilioni 329 Mradi Bwawa la Kidunda
Nov 11, 2022
Na Jacquiline Mrisho

Na Georgina Misama – MAELEZO

Serikali imeendelea kufanya jitihada mbalimbali ili kuimarisha sekta ya maji nchini ikiwa ni pamoja na kuhakikisha wananchi wanapata maji safi na salama, ambapo katika kukabiliana na changamoto ya upungufu wa maji katika Jiji la Dar es Salaam imeanza utekelezaji wa mradi wa ujenzi wa Bwawa la Maji la Kidunda.

Akizungumza leo jijini humo katika hafla ya uzinduzi wa Mradi wa Maji Kigamboni, Rais Samia Suluhu Hassan amesema kuwa Serikali inatambua kuwa mradi wa maji wa Kigamboni ni wa kupunguza makali ya changamoto hiyo na kwamba suluhisho la kudumu litatokana na mradi wa Bwawa la Kidunda ambalo litakapokamilika na kujazwa maji litaweza kuhudumia Jiji la Dar es salaam kwa miaka mitatu mfululizo.

“Uwepo wa Bwawa hili umeongelewa kwa muda mrefu, lakini leo ninayo furaha ya kwamba hatimaye sasa tunakwenda kujenga, tena kwa kutumia fedha zetu za ndani, mkataba tayari mkandarasi amekabidhiwa na leo mkandarasi atakwenda kuonyeshwa eneo litakapojengwa bwawa hilo ambalo tunatarajia litachua miezi 36 hadi likamilike,” amesema Rais Samia.

Aidha, Rais Samia amesema kuwa hadi kukamilika ujenzi wa bwawa hilo utagharimu shilingi bilioni 329 ambapo kiasi cha shilingi bilioni 100 kimeshatolewa na kuahidi kuendelea kutoa fedha kadri ujenzi unavyoendelea, aidha, amemtaka Waziri mwenye dhamana kumsimamia vyema mkandarasi ili akamilishe kazi hiyo kwa wakati na viwango vilivyokubalika.

Katika hafla hiyo, Rais Samia amekabidhi mitambo ya kuchimbia maji yenye thamani ya shilingi bilioni 35 na kusema kuwa fedha ambayo ingeelekezwa kwingine ingefanya jambo kubwa lakini Serikali imeamua kununua mitambo kwenda kufanya kazi ya kuchimba mabwawa sio tu kwa ajili ya wanadamu lakini kwa ajili pia ya mifugo.

“Mitambo ya uchimbaji visima na ujenzi wa mabwawa ninayoikabidhi ni imani yangu kwamba Wizara itaweza kusimamia jambo hili na imani hii iwe chachu ya viongozi wa Wizara na Taasisi zake kufanyakazi kwa bidii, uaminifu na weledi ili kutimiza kauli ya kumtua mama ndoo kichwani,” amesisitiza Rais Samia.

Mipangilio
Marekebisho ya Mandhari
Marekebisho ya Maandishi