Serikali imeeleza kuwa haiwezi kuhamisha jukumu la kulipa pensheni ya Wastaafu wa Shirika la Posta na Simu wa iliyokuwa Jumuiya ya Afrika Mashariki kwenda kwenye mojawapo ya Mifuko ya Hifadhi ya Jamii kwa kuwa zoezi la kuunganisha Mifuko ya Pensheni halijakamilika.
Hayo yamesemwa Bungeni Mjini Dodoma na Naibu Waziri wa Fedha na Mipango Mhe. Dkt. Ashatu Kijaji (Mb), wakati akijibu swali la msingi la Mbunge wa Ludewa Mhe. Deo Ngalawa (CCM), aliyetaka kufahamu, lini Serikali itakuwa tayari kuhamisha jukumu la kuwalipa Wastaafu wa lililokuwa Shirika la Posta na Simu la Afrika Mashariki kwenye moja wapo ya Mifuko ya Hifadhi ya Jamii.
Akijibu swali hilo, Naibu Waziri wa Fedha na Mipango, Dkt. Ashatu Kijaji alisema kuwa Serikali kupitia Shirika la Posta inaendelea na jukumu la kuwalipa pensheni ya kila mwezi Wastaafu wa shirika hilo.
“Uamuzi wa kuhamisha au kuendelea na utaratibu wa sasa utatolewa baada ya zoezi la kuunganisha mifuko ya pensheni kukamilika”, alisema Dkt. Kijaji.
Katika maswali ya nyongeza Mhe. Ngalawa alihoji kwakuwa Shirika la Posta limekuwa likisuasua katika kujiendesha na miongoni mwa mambo yanayosababisha ni ulipaji wa pensheni za Wastaafu hao, Serikali haioni ni wakati wa kulitua mzigo Shirika hilo na kuchukua jukumu hilo.
Mhe. Ngalawa alieleza kuwa kuanzia mwaka 2015 malipo ya pensheni kwa Wastaafu yalipanda kutoka Sh. 50,000 hadi Sh. 100,000 lakini kuna baadhi ya Wastaafu hawajabadilishiwa pensheni zao. Alitaka kujua lini Serikali itabadilisha pensheni hizo ili ziwe sawa kwa wote.
Dkt. Kijaji alisema kuwa baada ya Shirika la Posta kulipa Wastaafu huwasilisha madai yake Hazina na Serikali imekuwa ikirejesha fedha hizo kwa wakati na hakuna madai ya ziada.
Alifafanua kuwa Serikali kupitia Mifuko yote ya Hifadhi ya Jamii imekuwa ikilipa ongezeko la pensheni kwa Wastaafu kwa wakati, na kukiri kuwa Wastaafu wachache wamekuwa wakipeleka kesi za kutoongezewa pensheni zao kutokana na sababu mbalimbali.
Dkt. Kijaji alisema kuwa Hazina imekuwa ikipokea malalamiko hayo na kuyashughulikia, ametoa wito kwa Wastaafu wote yenye malalamiko wafike Hazina ili waweze kusaidiwa.