Na. Farida Ramadhani na Peter Haule, WFM, Dodoma
Serikali imeupatia Mfuko wa Hifadhi ya Jamii kwa Watumishi wa Umma (PSSSF) Shilingi trilioni 2.17 ikiwa ni malipo ya awamu ya kwanza ya deni la wastaafu walioanza kazi kabla ya mwezi Julai mwaka 1999, kupitia utaratibu wa Hati fungani maalum kwa ajili ya kuuwezesha mfuko huo kulipa mafao ya wastaafu kwa wakati na kuongeza mapato yake.
Hafla ya utiaji saini wa makubaliano hayo imefanyika jijini Dodoma kati ya Katibu Mkuu wa Wizara ya Fedha na Mipango na Mlipaji Mkuu wa Serikali, Bw. Emmanuel Tutuba na Mkurugenzi Mkuu wa PSSSF, CPA. Hosea Kashimba.
Akizungumza katika hafla hiyo Katibu Mkuu wa Wizara ya Fedha na Mipango, Bw. Emmanuel Tutuba alisema Serikali imeamua kutoa dhamana hiyo baada ya deni hilo kusababisha hitilafu kwenye mizania ya rasilimali za Mfuko huo ikilinganishwa na wajibu wa ulipaji mafao, kwa kuwa Mfuko huo umekuwa ukifanya malipo kwa kuzingatia kipindi chote cha ajira ya mstaafu kikiwemo kipindi cha kabla ya Julai 1999 cha kuanzishwa kwa mfuko huo.
“PSSSF ilianzishwa kufuatia kuunganishwa kwa mifuko minne (4) ya Pensheni ukiwemo mfuko wa PSPF ambao ulianzishwa mwaka 1999 na kuanza kulipa mafao mwaka 2004 kwa kuzingatia kipindi chote cha ajira ya mstaafu kikiwemo kipindi cha kabla ya Julai 1999, maana yake mstaafu wa mwaka 2004 aliyeajiriwa mwaka 1970, alilipwa na Mfuko kipindi chote cha ajira yake”, alifafanua Bw. Tutuba.
Alisema kwa kuwa kulikuwa na makubaliano na Serikali wakati wa uanzishaji wa Mfuko wa PSPF na kwa kuzingatia utaratibu wa kisheria kabla ya mwaka 1999, Serikali imeona ni sahihi kufanya malipo hayo kwa nia njema ya kuhakikisha sekta hiyo muhimu inaendelea kuhudumia Watanzania na kushiriki vyema kwenye ujenzi wa uchumi.
Bw. Tutuba alisema kuwa kukamilika kwa zoezi hilo ni utekelezaji wa agizo la Mhe. Rais Samia Suluhu Hassan, la kuhakikisha suala la ucheleweshwaji wa mafao ya wastaafu wa PSSSF linafanyiwa kazi kwa haraka ili punde mtumishi anapostaafu apatiwe mafao yake na mwezi unaofuata aanze kupokea pesheni yake ya kila mwezi.
Bw. Tutuba alisema Serikali inatumaini kuwa fedha hizo zilizotolewa, zitasaidia katika kulipa mafao ya wanachama wanaostaafu kwa wakati, kuendelea kulipa pensheni za mwezi kwa wastaafu na kutumika katika uwekezaji wenye tija ambao utasaidia kukuza thamani ya Mfuko.
Aidha, aliutaka mfuko huo kuongeza ufanisi na kuhakikisha unawafikia wanachama wake wote nchini hususani wale waliopo vijijini na maeneo yasiyofikika kwa urahisi ili waweze kunufaika na huduma.
Kwa upande wake Mkurugenzi Mkuu wa Mfuko wa Hifadhi ya Jamii kwa Watumishi wa Umma (PSSSF), CPA. Hosea Kashimba, aliishukuru Serikali ya Awamu ya Sita kwa kuweza kushughulikia suala la michango ambayo haikuwasilishwa kwa uliokuwa Mfuko wa PSPF kwa jina maarufu la “Pre 1999 liability”.
“Tunakuhakikishia kuwa kila kiasi tutakachopokea kitaelekezwa kwenye maeneo kusudiwa yakiwemo ya uwekezaji ili kuongeza thamani na ukwasi wa Mfuko, lakini pia jukumu kuu la ulipaji wa mafao kwa wakati kwa wanachama wetu wanaostahili kulipwa” aliahidi CPA. Kashimba.
Akizungumzia historia ya Mfuko huo, CPA. Kashimba alisema PSSSF ilianzishwa kwa Sheria ya Mfuko wa Hifadhi ya Jamii kwa Watumishi wa Umma Na. 2 ya Mwaka 2018 kufuatia kuunganishwa kwa mifuko ya Pensheni wa LAPF, PPF, GEPF na PSPF ambapo baada ya kuanzishwa kwake ulirithi mali na madeni yote ya mifuko iliyounganishwa.