Na Munir Shemweta, WANMM Mwanza
Serikali imetoa mwezi mmoja kuanzia Oktoba 19, 2022 kufanyika tathmini ya kina kwenye eneo lenye mgogoro wa ardhi linalozunguka uwanja wa ndege wa Mwanza.
Mgogoro huo unahusisha wananchi na Mamlaka ya Viwanja vya Ndege Tanzania (TAA) na Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ).
Hayo yamebainishwa jana katika Kata ya Shibula wilayani Ilemela Mkoa wa Mwanza na Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Dkt. Angeline Mabula wakati Kamati ya Mawaziri Nane wa Wizara za Kisekta ilipotembelea eneo hilo ikiwa ni sehemu ya ziara ya kamati hiyo kwenye mikoa mbalimbali nchini kuhusu utatuzi wa migogoro ya matumizi ya ardhi katika vijiji 975.
"Sasa tathmini ya kina itafanyika ndani ya mwezi mmoja, tunapoondoka hapa wataalamu wa timu ya kitaifa watapita nyumba baada ya nyingine kwa mitaa yote kufanya tathmini ya kina ndani ya mwezi mmoja tupate majibu" alisema Dkt. Mabula.
Dkt. Mabula ambaye ni kiongozi wa Kamati ya Mawaziri Nane wa Wizara za Kisekta aliwaambia wananchi kwenye mkutano huo kuwa, Serikali ya Awamu ya Sita haikutaka kuchukua uamuzi wa mwaka 2019 mojamoja na badala yake imerudi kwa wananchi wa maeneo hayo ili kupata ushauri wa changamoto za eneo hilo kabla ya kutoa maamuzi.
"Lengo hapa la kuja kwa timu ya kitaifa kufanya tathmini ni kujua nani ni nani na aliingia kwa wakati gani yote yatapatikana ndani ya mwezi mmoja", alisema Waziri Mabula.
Kwa mujibu wa Waziri wa Ardhi, Dkt. Angelina Mabula alisema ushauri utakaotolewa na kamati yake baada ya timu ya mkoa kujiridhisha pamoja na kamati ya wataalamu kupitia tena eneo hilo, kamati ya Mawaziri wa Wizara za Kisekta itatoa taarifa yenye maslahi kwa watanzania wote.
Ameitaka timu ya wataalamu kupewa nafasi na ushirikiano ili iweze kufanya kinachostahili ikiwemo kuonesha uthibitisho mbalimbali kama vile nyaraka na hatua zote za kiserikali zitafuatwa.
Kumbukumbu kuhusiana na mgogoro wa ardhi eneo la uwanja wa ndege wa Mwanza zinaonesha kiwanja hicho kilipimwa mwaka 1987 kikiwa na ukubwa wa hekta 1,470 kwa kuzingatia eneo lililokuwa limelipwa fidia kati ya mwaka 1978 hadi 1980
Hata hivyo mwaka 2003 hadi 2004, Mamlaka ya Viwanja vya Ndege Tanzania (TAA) ilijenga uzio kuzunguka eneo la kutua na kurukia ndege pamoja na miundombinu iliyopo ili kuimarisha usalama wa kiwanja cha ndege ambapo wakati wa ujenzi wa uzio iligundulika eneo pekee la kiwanja cha ndege lililovamiwa na wananchi ilikuwa ni mtaa wa Nyagungulu kata ya Ilemela.
Baada ya ujenzi wa uzio kulitokea tafsiri potofu kwa wananchi wakidhani kuwa mwisho wa mipaka ya kiwanja cha ndege ni uzio huo na kupelekea kuanza kuvamia eneo la kiwanja ambako kuna mitaa ya mhonze b, kihili, nyamilolelwa, shibula na bulyankhulu katika kata ya shibula.