Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Blogu ya Idara ya Habari - MAELEZO

Serikali Yatenga Bilioni 22.9 Kukarabati Vivuko Nchini
Dec 14, 2022
Serikali Yatenga Bilioni 22.9 Kukarabati Vivuko Nchini
Na Alfred Mgweno (TEMESA TANGA)

Serikali kupitia Wakala wa Ufundi na Umeme Tanzania (TEMESA) imetenga kiasi cha Shilingi bilioni 22.9 kwa ajili ya kuvifanyia ukarabati mkubwa vivuko 14 na kukarabati miundombinu ya vivuko katika maeneo 11 hapa nchini kwa gharama ya Shilingi bilioni 4.1. Hayo yamebainishwa leo wilayani Pangani mkoani Tanga wakati wa hafla fupi ya kupokea kivuko cha MV. TANGA ambacho kilikuwa kikifanyiwa ukarabati mkubwa baada ya kufikia muda wake wa ukarabati mapema mwezi Juni mwaka huu ambapo kiliondolewa kwenye maji na kukabidhiwa kwa Mkandarasi Dar es Salaam Merchant Group.

Akizungumza katika hafla hiyo, mgeni rasmi, Mkuu wa Mkoa wa Tanga, Mhe. Omar Mgumba ameipongeza Serikali ya Awamu ya Sita kwa kuweza kutekeleza mradi huo huku ikitumia fedha za ndani na kuongeza kuwa kukamilika kwa ukarabati wa kivuko cha MV. TANGA kutaboresha huduma za usafiri wa bidhaa mbalimbali kwa wananchi wa maeneo ya Pangani na Mkoa wa Tanga kwa ujumla hivyo kuongeza kasi ya maendeleo na ukuaji kiuchumi kwa wananchi.

‘‘Kukamilika kwa ukarabati wa kivuko MV Tanga kutaboresha huduma za mawasiliano na usafirishaji na hivyo kuongeza kasi ya maendeleo na ukuaji kiuchumi kwa wananchi, nitoe pongezi kwa Wizara ya Ujenzi kwa kuwezesha ujenzi wa vivuko vipya vinavyojengwa nchini kama alivyoeleza Mtendaji Mkuu wa TEMESA pamoja na kupongeza jitihada zinazochukuliwa katika ukarabati wa vivuko mbalimbali kwani kufanya hivyo kutaongeza huduma za usafiri majini nchini‘‘, amesema Mhe. Mgumba.

Naye Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Ufundi na Umeme Tanzania (TEMESA), Lazaro Kilahala, akizungumza katika hafla hiyo, amesema katika mwaka wa fedha 2022/23, TEMESA kupitia Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi inatekeleza miradi mbalimbali ya ujenzi na ukarabati wa vivuko na miundombinu yake ikiwa ni muendelezo wa utekelezaji wa Ilani ya Uchaguzi ya Chama cha Mapinduzi ya mwaka 2020-2025.

‘’Ukarabati wa Kivuko cha MV. TANGA umegharimu kiasi cha Shilingi 1,118,092,480.00 (pamoja na VAT), aidha, katika mwaka huu wa fedha Serikali inavifanyia ukarabati vivuko 14, kikiwemo cha MV. TANGA MV. MISUNGWI, MV. MUSOMA, MV. SABASABA, MV. KAZI, MV. NYERERE, MV. KITUNDA, MV. KILOMBERO II, MV. RUHUHU, MV. OLD RUVUVU, MV. MAGOGONI, MV. UJENZI, MV. KOME II, na MV. MARA’’. Alisema Kilahala.

Aidha, Mbunge wa Pangani, Mhe. Juma Aweso ameishukuru Serikali ya Awamu ya Sita kwa kuwezesha ukarababati wa kivuko hicho kufanyika na kuipongeza TEMESA na Wizara ya Ujenzi kwa kusimamia ukarabati wa kivuko hicho kwa umakini.

‘’Nitumie nafasi hii kumshukuru Rais wangu Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kazi kubwa na nzuri anayoifanya si nchini tu lakini katika jimbo langu la Pangani, nitumie nafasi hii pia kukupongeza Naibu Katibu Mkuu, Waziri wa Ujenzi na watendaji wote, upo hapa Mtendaji Mkuu wa TEMESA, mmetutendea haki sana wana Pangani.’’ Alisema Mhe. Aweso.

Naye Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Ujenzi, Mhe. Ludovick Nduhiye akizungumzia kuhusu changamoto zinazoikumba TEMESA, ameiomba Serikali kuangalia suala la kupandisha nauli za vivuko kwa kuwa nauli hizo ni za zamani na zimepitwa na wakati, ‘’Jambo lingine ambalo tunaliangalia Wizara, TEMESA na wadau mbalimbali ni suala la nauli kuwa bado za chini, nauli hizi zimeandaliwa kama miaka kumi iliyopita, mambo yamebadilika sana lakini tunawasiliana na mamlaka husika kwa kushirikiana na wananchi ili tuone ni namna gani tunaweza kupandisha nauli hizo.’’ Alimaliza Naibu Katibu Mkuu.

Mtendaji Mkuu TEMESA, Lazaro Kilahala ameishukuru Serikali ya Awamu ya Sita chini ya Mhe. Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kupitia Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi kwa kuuwezesha Wakala kifedha kutekeleza mradi huo na kuahidi kufanya kazi kwa weledi na jitihada kubwa ili kufikia malengo na matarajio ya Serikali na wanachi kwa ujumla.

Kivuko cha MV. TANGA kina uwezo wa kubeba abiria 100 na magari 6 sawa na tani 50.

Mipangilio
Marekebisho ya Mandhari
Marekebisho ya Maandishi