[caption id="attachment_42965" align="aligncenter" width="750"] Naibu Katibu Mkuu wa Ofisi ya Makamu wa Rais, Balozi Joseph Sokoine akitoa ufafanuzi kuhusu marufuku ya matumizi ya mifuko ya plastiki wakati akiongea na Waandishi wa Habari leo Jijini Dodoma. Serikali imepiga marufuku matumizi na biashara ya mifuko ya plastiki ifikapo tarehe 1 Juni, 2019. Kushoto ni Kaimu Mkurugenzi wa Idara ya Mazingira, Kanizio Fredrick Manyika.[/caption]
Na: Frank Shija, MAELEZO Dodoma.
Serikali yasisitiza marukufu ya matumizi ya mifuko ya plastiki ifikapo tarehe 1 Juni 2019 ipo palepale tofauti na inavyopotoshwa na baadhi ya watu wenye nia hovu ya kuleta mkanganyiko miongoni mwa jamii.
Hayo yamesemwa na Naibu Katibu Mkuu wa Ofisi ya Makamu wa Rais, Muungano na Mazingira, Balozi Joseph Sokoine alipokuwa akiongea na Waandishi wa Habari leo jijini Dodoma.
Alisema kuwa katazo hilo la kupiga marufuku mifuko ya plastiki ya aina zote lilitolewa na Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa wakati akihitimisha Hotuba yake ya Bajeti ya Ofisi ya Waziri Mkuu.
“Mtakumbuka kuwa tarehe 9 Aprili 2019 Serikali ilitoa Tamko la kusitisha matumizi ya Mifuko ya plastiki hapa nchini ifikapo Juni Mosi 2019, katazo hili linalenga kuepusha athari za kiafaya na mazingira zinazoendelea kujitokeza kutokana na matumizi ya mifuko hiyo” alisema Balozi Sokoine.
Balozi Sokoine amesema kuwa wananchi wanapaswa kuunga mkono jitihada hizo na si kubeza na kupotosha kama ambavyo imetokea hivi karibuni kwa mtu kutumia video clip kwa kuisambaza mitandaoni kwa lengo la kupotosha umma.
“Nitumie fursa hii kuwakumbusha wananchi wote kuwa ifikapo tarehe 1 Juni 2019, Serikali itaendesha operesheni kabambe nchi nzima ya kusaka mifuko hii, ambayo itahusisha wadau mbalimbali vikiwemo Vyombo vya Ulinzi na Usalama, Kamati za Ulinzi na Usalama za Mikoa na Wilaya, Mamlaka za Serikali za Mitaa Mamlaka ya Maabara ya Mkemia Mkuu wa Serikali, TBS, TFDA, Ofisi ya Mashtaka, pamoja na Mamlaka za Viwanja vya Ndege,Bandari, Forodha, Uhmiaji, na Usafiri wa Nchi Kavu,”
Aliongeza kuwa katika kufanikisha zoezi hilo Serikali imeshafanya maandalizi mbalimbali ikiwemo kutunga kanuni zitakazo anza kutumika kuanzia tarehe 1 Juni, 2019 hivyo ametoa rai kwa watanzania wote kuzingatia maelekezo ya Serikali pamoja na matakwa ya Kanuni za kupiga marufuku matumizi na biashara ya mifuko ya plastiki nchini kwa mustakabali wa uhifadhi wa mazingira ya nchi yetu.