Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Blogu ya Idara ya Habari - MAELEZO

Serikali Yashusha Tozo Bandari za Tanga, Mtwara, Yataja Mikakati ya Uboreshwaji Iliyofanywa.
May 19, 2022
Na Jacquiline Mrisho

Na Mawazo Kibamba, MAELEZO

Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Kassim Majaliwa amesema katika msimu uliyopita, Serikali imefanya mapitio ya tozo katika Bandari za Tanga na Mtwara na kutoa punguzo la asilimia 30% kwa meli yoyote inayoshusha na kupakia mizigo kwenye bandari hizo.

Amesema lengo ni kuvutia matumizi ya bandari hizo na kuzipa urahisi nchi jirani na bandari hizo ambazo zimefanyiwa maboresho makubwa ya kuweza kupokea mzigo wowote.

Waziri Mkuu alikuwa akijibu maswali ya papo kwa papo yaliyoulizwa na baadhi ya Wabunge, ambapo Mbunge wa Nanyamba, Mhe. Abdallah Chikota alitaka kujua mkakati wa Serikali wa kuzitangaza fursa za bandari zilizopo nchini.

Akijibu swali hilo, Waziri Mkuu amesema Serikali imetenga fedha kwa ajili ya maboresho ya bandari zote nchini, ikiwemo zile zilizopo kwenye Bahari Kuu na kwenye Maziwa Makuu na kuimarisha miundombinu na huduma mbalimbali.

“Ni kweli kwamba Serikali yetu kupitia Rais wetu Samia Suluhu Hassan imetenga fedha kwa ajili ya maboresho ya bandari zote nchini, ikiwemo zile zilizopo kwenye Bahari Kuu na zilizopo kwenye Maziwa Makuu, ili kuimarisha miundombinu na huduma mbalimbali, mkakati wa Serikali wa namna ya kuvutia matumizi ya bandari hizi kwa nchi jirani ipo, na inasimamiwa na Wizara yetu ya Ujenzi na Uchukuzi, kwanza tunaongeza vifaa vinavyoweza kupakua na kupakia mizigo kwa muda mfupi, ili kuwahakikishia wateja wetu kuwa matumizi ya bandari hizi yanatumia muda mfupi zaidi” amesema Waziri Mkuu.

Amesema Bandari za Tanga na Mtwara pamoja na bandari zingine zimekuwa ni kichocheo kikubwa cha uchumi na hivyo Serikali imeona ni muhimu kuzitumia ili kuongeza pato la Taifa na la mwananchi mmoja mmoja.

“Tumefanya mapitio ya tozo hasa kule Tanga na Mtwara tumetoa fursa ya kupunguza tozo ili kuvutia, ukilinganisha na Dar es Salaam kwa sababu bandari ya kule idadi ya meli ni kubwa sana ukilinganisha na Tanga na Mtwara, hata msimu uliopita tulilishughulikia hili na tulipunguza tozo ya asilimia 30 ya meli yoyote inayokwenda Tanga kwa ajili ya kuwezesha nchi kama Somalia, Sudan ili kuweza kutumia bandari ya Tanga na kule Mtwara, nchi kama Malawi, Zambia na hiyo Congo, ambako ni rahisi kufika ili wateja wale wanaoleta mizigo katika bandari hizi waweze kuvutiwa zaidi” amesema Waziri Mkuu.

Ametoa wito kwa wafanyabiashara wa ndani na nje ya nchi kutumia bandari zilizoko ukanda wa Pwani na kwenye Maziwa makuu na kuwahakikishia usalama wa mali zao.

Waziri Mkuu pia amesema Serikali katika msimu wa kilimo uliopita haijawahi kuweka zuio kwa Wakulima kuuza mahindi nje ya nchi bali iliweka utaratibu ambao uliruhusu wakulima hao kuuza ziada ya zao hilo, hatua ambayo ililenga kuhakikisha nchi inakuwa na usalama na ziada ya chakula.

Akijibu swali la Mbunge wa Mbinga Vijijini Mhe. Benaya Kapinga, aliyeuliza kuwa, mwaka jana nchi yetu ilikumbwa na tatizo kubwa la soko la mahindi, hali iliyopelekea Wakulima wa Mikoa ya Mbeya, Ruvuma, Njombe, Iringa na Rukwa kuuza zao hilo kwa shilingi elfu 15 kwa gunia, na hii ilitokana na baadhi ya Wakulima kudhani kwamba kuna zuio la kuuza zao hili nje ya nchi, nini kauli ya Serikali kuhusu zao hili kwa wakulima? ambapo Waziri Mkuu amesema lengo lilikuwa ni kujihakikishia usalama wa chakula.

“Niwapongeze na kuwashukuru sana Wakulima wa maeneo haya, kwa sababu leo hii tunaposema tuna uhakika na usalama wa chakula kwa maana ya kuwa na kiwango kikubwa cha chakula ni kutokana na wakulima hawa, ni kweli zao la mahindi mwaka jana tulipata changamoto kwa sababu bei ilishuka, wakulima wengi walidhani tumeweka zuio la kupeleka mahindi nje, serikali haina zuio hilo, tunachokifanya ni lazima tujiridhishe na kiwango cha chakula na ile ziada ndiyo tunaruhusu iuzwe nje, kwa hiyo hata msimu huu Wizara ya Kilimo ikishafanya tathmini zake na kujua kiwango cha chakula tulichonacho na kuitambua ile ziada, tutatoa kibali cha kuuza nje ili wakulima wapate masoko ya uhakika, sasa utaratibu tunaoutumia hapa hatupeleki nje holela, yule mkulima anayetaka kupeleka nje, aombe tu kibali kwa Mkuu wa Wilaya.” Amesema Waziri Mkuu. 

Katika hatua nyingine Wabunge wameendelea na maswali katika Wizara za Ujenzi na Uchukuzi, Wizara ya Afya na Wizara ya mambo ya ndani ya nchi.

Mipangilio
Marekebisho ya Mandhari
Marekebisho ya Maandishi