Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania inayoongozwa na Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan imeendelea kupongezwa kwa jitihada zake za kutekeleza miradi mbalimbali ya maendeleo inayolenga kuboresha maisha ya Watanzania.
Wakazi wa Wilaya ya Lindi kutoka maeneo mbalimbali wakizungumza leo na Afisa Habari wa Idara ya Habari - MAELEZO wamepongeza utekelezaji wa miradi ya kimkakati inayofanywa na Serikali katika mkoa wao.
Mkazi wa Tulieni, Bw. Issa Omary amesema kuwa Mkoa wa Lindi umepata neema ya miradi mbalimbali ambayo wanaamini itaendelea kubadilisha maisha yao.
"Uwepo wa Hospitali ya Rufaa hapa kwetu unatusaidia kwa sababu awali tulikua tunatibiwa katika Hospitali ya Sokoine ambayo iko mbali kutoka hapa", amebainisha Bw. Issa.
Naye, Mkazi wa Kata ya Mwenge, Bi. Neema Nasoro amesema "Tunaipongeza Serikali kwa kujenga shule hii ya kisasa ya Sekondari ya Wasichana Lindi itasaidia watoto wetu kusoma bila kusafiri umbali mrefu kwenda Shule ya Mitwero, hivyo uwepo wake utasaidia sana watoto wa kike kutimiza ndoto zao".
Ameongeza "Tumefurahi kwa Serikali kujenga Bandari ya kwanza ya Uvuvi hapa Kilwa ni matumaini yangu itasaidia kukuza shughuli za sekta ya uvuvi nchini".