Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Blogu ya Idara ya Habari - MAELEZO

Serikali Yapongezwa Mazingira Rafiki Ya Uwekezaji
Dec 12, 2018
Na Msemaji Mkuu

Na:  Beatrice Lyimo

Serikali ya Awamu ya Tano inayoongozwa na Rais Dkt. John Magufuli yapongezwa kwa kuonesha ushirikiano na uthamini kwa wawekezaji nchini.

Pongezi hizo zimetolewa na Mkurugenzi wa Masuala ya Ushirikiano na Uhusiano wa Jamii wa Kampuni ya Cetawico Limited, Bi. Katrin Boehl  jana Jijini Dodoma wakati alipotembelewa na Waandishi wa Habari za Uchumi na Fedha.

"Kwa upande wangu lazima niseme nimeona ushirikiano wa hali ya juu  katika Serikali yangu Dodoma kwani nikiwa na tatizo lolote ninakwenda katika ofisi za Serikali yangu ya Dodoma hivyo imeonesha uthamini wa kiwango kikubwa wa  kazi tunazofanya" ameongeza Bi. Katrin.

Lengo la Waandishi wa Habari za Uchumi na Fedha kutembelea Kiwanda hicho ni  kujifunza kwa vitendo shughuli za kiuchumi zinazofanywa katika jiji la Dodoma ikiwa ni utekelezaji wa agenda kuu ya Serikali ya Awamu ya Tano kuhusu Uchumi wa Viwanda.

Kabla ya ziara hiyo mada mbalimbali ziliwasilishwa na wawezeshaji kutoka Benki Kuu ya Tanzania (BoT) kwa Waandishi hao ikiwemo Uwekezaji katika dhamana za Serikali; faida zake kwa taifa na Wawekezaji.

Akiwasilisha mada hiyo Mkurugenzi wa Masoko ya Fedha wa Benki Kuu ya Tanzania (BoT), Bw. Alexander Ng’winamila amesema kuwa Serikali  inakopa nje ya nchi pale inapotokea  kwamba soko la ndani la kukopa halitoshelezi  mahitaji yonayohitajika kwa wakati huo.

"Sababu kubwa inayoweza kupelekea Serikali kukopa nje na sio ndani ya nchi ni pale miradi au mipango mbalimbali ya maendeleo iliyo nayo ni mikubwa ikiliganishwa na  uwezo wa soko kutoka ndani ya nchi.

Aidha,  Bw. Ng’winamila amesema kuwa kuna aina mbili za  dhamana za serikali ambapo ni dhamana za muda mfupi yaani (Treasury Bills) ikiwa  Serikali inakopa kutoka kwa wananchi katika kipindi kisichozidi mwaka mmoja, zipo za siku 35,91,182 na 364 na dhamana za serikali za muda mrefu (Treasury Bonds) ambazo huiva katika kipindi kinachozidi miaka 2, 5,7,10 na 20.

"Ushiriki katika minada ya dhamana za serikali uko wazi kwa raia wa Jumuiya ya Afrika Mashariki zikiwemo taasisi kama Mifuko ya Hifadhi ya Jamii, Mabenki na watu binafsi wa kada zote wakiwemo wajasiriamali wadogo" alisema Bw. Ng’winamila.

Mbali na hayo Meneja kutoka Kurugenzi ya Usimamizi wa Sekta ya Fedha BoT, Bw. Nassor Omary amewasisitiza Waandishi wa Habari za kibenki   kuwa waaminifu, kufuata maadili na kufanya utafiti ili kutoa habari zilizothibitishwa kwani wana wajibu wa kutoa habari ambazo zitajenga taasisi za fedha na uchumi kwa ujumla.

Bw. Nassor  ameyasema hayo wakati akiwasilisha mada kuhusu Umuhimu wa Waandishi wa Habari kwa Taasisi za Fedha na kusema kuwa Waandishi wa Habari wana umuhimu mkubwa wa kutoa taarifa kwa jamii ili iweze kufanya maamuzi sahihi kwa maisha yao.

"Waandishi wa Habari hasa za kibenki wanapaswa kufahamu kuwa Mfumo wa fedha unafanya sehemu muhimu ya uchumi wa nchi na hofu yeyote kwenye sekta ya kibenki inawea kuporomosha uchumi" amesisitiza Bw. Nassor.

Benki Kuu ya Tanzania inaendesha semina kwa Waandishi wa Habari za Uchumi na Fedha kwa lengo la kujengea uwezo wa kuweza kusoma, kuchambua na kuziandikia taarifa na takwimu mbalimbali zinazotolewa na BoT.

 

Mipangilio
Marekebisho ya Mandhari
Marekebisho ya Maandishi