Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Blogu ya Idara ya Habari - MAELEZO

Serikali Yapongezwa Sheria Upatikanaji wa Taarifa.
Sep 28, 2017
Na Msemaji Mkuu

Na: Thobias Robert

Serikali ya awamu ya tano inayoongozwa na Rais Dkt. John Pombe Magufuli imepongezwa kwa kupitisha Sheria ya haki ya upatikanaji wa habari kutoka katika taasisi na mashirika ya umma pamoja na binafsi hapa nchini.

Pongezi hizo zimetolewa Jijini Dar es Salaam jana na Jaji Mstaafu Amiri Manento ambaye pia aliwahi kuwa Mwenyekiti wa  Tume ya Haki za Binadamu na Utawala bora, alipokuwa katika  maadhimisho ya siku ya  Kimataifa ya Upatikanaji wa Taarifa iliyofanyika katika ukumbi wa   Millenium Tower.

“Kwa mujibu wa Katiba kila Mtanzania anayo haki ya kupewa taarifa wakati wowote kuhusu matukio mbalimbali na muhimu kwa maisha ya wananchi kuhusu masuala ya kijamii na kimaendeleo, hivyo mwaka 2016, Sheria ya kupata taarifa ilipitishwa na Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na kuidhinishwa na Rais John Pombe Magufuli ili kuwezesha wananchi kupata taarifa,” alifafanua Jaji Manento.

Aidha, aliongeza kuwa, hatua ya serikali ya kupitisha Sheria hiyo ni kuendana na mikataba na Sheria za kimataifa ambazo zinamtaka kila mwananchi kutoa, kupokea na kupata taarifa juu ya shughuli mbalimbali zinazoendelea  katika taifa lake,Tanzania ni mwanachama na imeridhia Sheria na mikataba hiyo itumike.

Jaji Manento alisema kuwa, Sheria ya kupata taarifa ina umuhimu mkubwa katika taifa kwani zaidi ya nchi 100 duniani zinazotumia sheria hii zimefanikiwa kupambana na vitendo viovu kama vile rushwa, matumizi mabaya ya madaraka kwa viongozi wa umma, ubadhilifu wa rasilimali za nchi, kuongeza uwazi na uwajibikaji kwa viongozi wa umma na taasisi binafsi pamoja na kukuza utawala bora.

Aliendelea kuongeza kuwa, nchi kama India na Mexico Sheria hii imewahi kuwakuta viongozi na hatia za ubadhilifu wa rasilimali za umma na matumizi mabaya ya madaraka yao hivyo kupelekea kufukuzwa kazi, kufilisiwa pamoja na kufungwa jela kwa mujibu wa Sheria za nchi hizo.

Mwenyekiti huyo mstaafu wa Tume ya haki za binadamu na utawala bora ametoa wito kwa serikali kuitungia sera na kanuni Sheria hiyo ili ianze kutumika hapa nchini  mara moja “Ningependa kuwakumbusha watumishi wa serikali hasa wale wanaohusika na utekelezaji wa Sheria hii, kuchukua hatua mahususi kuhakikisha kuwa kanuni zinatayarishwa na zinatagazwa kwenye gazeti la serikali,” alisisitiza.

Awali akizungumza katika maadhimisho hayo, Mwenyekiti wa Umoja wa Haki ya Kupata Taarifa (CoRI) Kajubi Mukajanga alisema kuwa kutungwa kwa Sheria ya upatikanaji wa taarifa ina umuhimu mkubwa katika taifa kwani inamhusu kila Mtanzania kupata na kutoa taarifa kwa ustawi wa mtu mmoja mmoja na taifa kwa ujumla.

“Sheria ya upatikanaji wa habari ni muhimu sana kwasbabu inamhusu kila mtu hasa kwa nyakati za sasa ambazo ni nyakati muhimu sana zinazohitaji mijadala ya kina na mijadala ya wazi kwasababu ya mustakabali wa kujenga taifa linaloongea na linaloruhusu upatikanaji wa taarifa,”  alifafanua Bw.Mukajanga.

Sherehe ya kuadhimisha siku ya upatikanaji wa taarifa huadhimishwa kila mwaka ifikapo Septemba 28, kufuatia kupitishwa na Umoja wa Mataifa mwaka 2002 katika mji wa Sophia Bulgaria. Kwa hapa nchini sherehe hii imefanyika kwa mara ya kwanza mwaka huu na kuhudhuriwa na wadau mbalimbali kutoka ndani na nje ya nchi, mashirika na taasisi za umma pamoja na binafsi.

Mipangilio
Marekebisho ya Mandhari
Marekebisho ya Maandishi