Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Mhe. William Lukuvi amepiga marufuku Halmashauri, Taasisi na watu binafsi kuchukua maeneo ya wananchi bila kulipa fidia.
Akizungumza hivi karibuni mkoani Singida wakati wa ziara yake ya kikazi katika mkoa huo, Lukuvi alisema kumekuwa na tabia ya baadhi ya Halmashauri na Taasisi kuchukua maeneo ya wananchi bila ya kuwalipa fidia kwa maelezo maeneo hayo kuhitajika kwa ajili ya shughuli za kimaendeleo.
Kwa mujibu wa Lukuvi, sheria inakataza kuchukua maeneo ya wananchi bila kulipa fidia na Mhe. Rais John Pombe Magufuli alishakataza kunyang'anya maeneo ya wananchi bila kulipa fidia.
Waziri Lukuvi alifikia kutoa maamuzi hayo baada ya kupokea malalamiko kutoka kwa Bibi Maria Samweli mkazi wa Singida ambaye alimpa malalamiko yake ya kutolipwa fidia kwa zaidi ya miaka 12 kwa ajili ya kupisha mradi wa upimaji na ugawaji viwanja.
"Mtu yeyote atakayeendeleza maumivu kwa wananchi kwa kuendeleza kero ya kuchukua maeneo bila kulipa fidia kazi yake itakuwa kubwa, kwanza msisitizo ulishawekwa na Mhe. Rais Magufuli aliyepiga marufuku wahusika kupora maeneo ya wananchi bila kulipa fidia" alisema Lukuvi.
Alisema, upo utaratibu wa kuchukua maeneo ya wananchi kwa manufaa ya umma na utaratibu huo lazima mwananchi alipwe fidia kwa kupewa haki yake na kusisitiza kuwa ardhi pekee inayoweza kuchukuliwa bila kulipa fidia ni ile aliyomilikishwa mtu kwa hati na mmiliki huyo akashindwa kuendeleza kwa wakati ambapo hati hiyo ikifutwa mmiliki wake hawezi kulipwa fidia.
Waziri Lukuvi aliongeza kuwa, Halmashauri yoyote ikitamani ardhi inayomilikiwa kihalali na hata kama halijaendelezwa lazima mmiliki wake alipwe fidia na kusisitiza kwamba, tangu mwaka 1999 ardhi isiyofanyiwa kitu chochote ina thamani yake na kilichoendelezwa juu yake nacho kina thamani yake.