Na. Fatma Salum.
Serikali kupitia Mamlaka ya Udhibiti wa Mbolea (TFRA) imepata mzabuni mpya ambaye ataagiza tani elfu ishirini za mbolea ya kukuzia aina ya UREA inatarajiwa kuingia nchini mwezi Februari mwaka huu.
Akizungumza katika kikao cha ufunguzi wa zabuni kilichofanyika jana jijini Dar es Salaam, Kaimu Mkurugenzi wa Mamlaka hiyo Bw. Lazaro Kitandu alisema kuwa lengo la kutangaza zabuni hiyo ni kuagiza mbolea ya ziada ili kuwa na mbolea itakayotosheleza msimu mzima.
“Zabuni hii ilitangazwa mapema Januari mwaka huu na leo tumepata mshindi atakayeleta mbolea hiyo ambaye ni kampuni ya ETG INPUTS LTD baada ya kukidhi vigezo vya zabuni hiyo,” alisema Kitandu.
Alieleza kuwa hiyo ni awamu ya pili kwa msimu huu kuagiza mbolea na kwamba mara mbolea hiyo itakapowasili itasambazwa nchi nzima hususan mikoa ya kaskazini kwa sababu katika maeneo hayo tayari msimu wa kilimo umeanza.
Kitandu alibainisha kuwa uagizaji wa mbolea ya muda mrefu unasaidia kuepuka athari ya kupanda kwa bei ya mbolea katika soko la dunia.
Alifafanua kuwa utaratibu wa kumpata Mzabuni wa kuagiza mbolea unatokana na mfumo wa ununuzi mbolea kwa pamoja ulioanza Julai mwaka jana kufuatia kanuni mpya za Sheria ya Mbolea ya mwaka 2009.
“Mfumo huu wa uagizaji mbolea kwa pamoja unanufaisha zaidi ya wakulima milioni 20 tofauti na utaratibu wa ruzuku uliokuwa unanufaisha wakulima milioni moja tu,” aliongeza Kitandu.
Pia alisema kuwa mbolea ya kwanza kuagizwa kupitia mfumo wa pamoja iliingia nchini Septemba 2017 ikiwa ni jumla ya tani elfu 55 za mbolea ya kupandia na kukuzia.
Akizungumzia hali ya upatikanaji mbolea nchini, Kitandu alibainisha kuwa kwa sasa mbolea inapatikana nchi nzima kwa sababu kazi ya usambazaji imeenda vizuri kwenye mikoa yote na bado inaendelea ili kuhakikisha kila mkulima anapata mbolea kadri ya mahitaji yake.
“Usambazaji wa mbolea umefanikiwa hasa kwenye maeneo yaliyokuwa na uhaba ambapo baadhi ya maeneo wamepata mbolea nyingi zaidi ya mahitaji yao,” alisema Kitandu.
Aidha, alifafanua kuwa kwenye baadhi ya maeneo ya vijijini ambako mbolea haijawafikia wakulima ni kutokana na changamoto ya mvua zinazoendelea kunyesha hivyo makampuni mengi yanayosambaza yalishindwa kufika kwa sababu ya miundombinu.
“Mbolea imefika kwenye halmashauri zote nchini ingawa kuna changamoto ya kufika vijijini kutokana na mvua zinazoendelea lakini Serikali imetoa maelekezo kwa Halmashauri zenye changamoto hiyo kuhakikisha mbolea inawafikia wakulima kila mahali,” alisema.
Kitandu alisema matarajio ya kuagiza mbolea kwa msimu ujao wa mwaka 2018/2019 ni kufikia tani 430,000 hadi 450,000.