Serikali inaendelea kufanya juhudi za makusudi ya kuongeza ushiriki wa vijana na wanawake katika sekta ya kilimo ili kuwaletea maendeleo yatokanayo na kilimo.
Kauli hiyo imetolewa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan leo jijini Mbeya wakati wa Kilele cha Maonesho ya Siku ya Wakulima ( Nanenane) yaliyofanyika kitaifa jijini humo.
Rais Samia amesema zipo programu na juhudi za makusudi za kuwawezesha wanawake na vijana katika kilimo.
"Miongoni wa juhudi hizo ni kuanzishwa kwa programu ya miaka 8 inayoitwa "Jenga Kesho Iliyobora" ambapo hadi sasa vijana 812 wanakidhi vigezo ikiwa ni wanawake 282 na wanaume 530 wanaendelea na mafunzo ya awamu ya kwanza," alisema Rais Samia.
Aliongeza kuwa baada ya kuhitimu mafunzo hayo vijana watapatiwa mashamba yenye kufikia hadi ekari 10 kulingana na mazao wanayokwenda kulima, mashamba hayo watakodishwa kwa miaka 66.
Juhudu zingine za makusudi ni serikali inaendelea kutafuta wawekezaji watakaokuwa wakinunua mazao hayo na kuyaongezea thamani.
Kwa mujibu wa Dkt. Samia juhudi hizi zimeifanya Tanzania kujulikana kimataifa na kuchaguliwa kuwa mwenyeji Jukwaa la Kilimo litakalofanyika Septemba 5 hadi 8, 2023.
Kufuatia jukwaa hilo Tanzania itapata fursa za kibiashara na kuimarisha mashirikiano na nchi za Afrika kwenye mifumo ya chakula.