Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Blogu ya Idara ya Habari - MAELEZO

Serikali Yakabidhi Mashamba 11 Yaliyoshindwa Kuendelezwa kwa Wananchi Kilosa
Aug 20, 2022
Na Jacquiline Mrisho

Na. Hassan Mabuye, Morogoro

Naibu Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Mhe. Ridhiwani Kikwete amekabidhi mashamba makubwa 11 ambayo hayakuendelezwa kwa muda mrefu kwa wakazi wa Wilaya ya Kilosa mkoani Morogoro kwa niaba ya Mhe. Rais Samia ili yaweze kutumika kwa kilimo.

Naibu Waziri Kikwete amekabidhi mashamba hayo mwishoni mwa wiki hii katika mkutano wa hadhara uliofanyika wilayani hapo kwa ajili ya kusikiliza kero za ardhi na kuwaeleza wakazi hao kuwa Mhe. Samia Suluhu Hassan ameelekeza mashamba hayo yagawiwe kwa wananchi na yapangiwe matumizi.

Aidha, Naibu Waziri Kikwete amewataka viongozi wa Wilaya ya Kilosa, Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Kilosa na Kamishna wa Ardhi Msaidizi Mkoa wa Morogoro kusimamia mpango wa matumizi ya mashamba hayo na kuyagawa kwa haki kama alivyoelekeza Mhe. Rais.

“mashamba haya Mheshimiwa Rais ameelekeza yakagawiwe kwa wananchi, kwa sababu alishayatwaa na sasa akatuelekeza sisi tuyapangie matumizi na mchakato huo wa kufanya matumizi ya kugawa mashamba hayo umeishakamilika” Amesema Mhe. Kikwete.

Naibu Waziri Kikwete amesisitiza kuwa mashamba hayo yagawiwe kwa wananchi kwa kuzingatia makundi yaliyoelekezwa ambayo ni vijana, wanawake na walemavu ili yatumike kwa ajili ya kilimo katika vikundi vya ushirika na kwa ajili ya uwekezaji.

Miongoni mwa mashamba hayo yaliyogawiwa kwa wananachi ni Noble Agricultural Enterprises LTD ekari 1,700, shamba la I. M. Nahdi ekari 1,235.7, shamba la New Msowelo Farms LTD ekari 609, shamba la Majambaa, Mbuga Sisal, Magole Sisal, mashamba ya Mvumi, mashamba ya Kimamba na shamba lililokuwa linamilikiwa na Mamlaka ya Mkonge.

Katika hatua nyingine Naibu Waziri Kikwete amekemea tabia ya wakazi wa Kilosa mkoani Morogoro na wakazi wa maeneo mengine ambao wakishagawiwa na kumilikishwa ardhi baadae huuza, jambo ambalo hupelekea migogoro na malalamiko mara kwa mara.

Mipangilio
Marekebisho ya Mandhari
Marekebisho ya Maandishi