Serikali imesema itaendelea kutafuta fedha za kutekeleza miradi mbalimbali ya kukabiliana na athari za Mabadiliko ya Tabianchi kwa pande zote mbili za Muungano.
Hayo yamesemwa leo Agosti 3, 2022 na Naibu Katibu Mkuu Ofisi ya Makamu wa Rais (Mazingira), Dkt. Switbert Mkama alipofanya ziara ya kikazi ya kukagua utekelezaji wa Mradi wa Kuhimili Mabadiliko ya Tabianchi kwa kutumia Mifumo Ikolojia Vijijini – EBARR unaotekelezwa katika Wilaya ya Kaskazini ‘A’ Unguja na kusimamiwa na Ofisi ya Makamu wa Rais.
Akiwa katika eneo la Mbuyutende, Dkt. Mkama ametoa rai kwa wanufaika wa mradi wa boti 6 za uvuvi zilizotolewa kupitia Mradi wa Kuhimili Mabadiliko ya Tabianchi kwa Kutumia Mifumo Ikolojia Vijijini (EBARR) kutumia boti hizo katika shughuli za uvuvi na utalii kama shughuli mbadala ya kujiongezea kipato na kutofanya shughuli zinazochangia uharibifu wa mazingira kama vile kuchoma mkaa.
Boti hizo zenye thamani ya Shilingi milioni 162, zina uwezo wa kubeba mizigo kiasi cha tani 2.9 kwa wakati mmoja na zimekabidhiwa kwa vikundi vya wavuvi katika Shehia tatu za Matemwe.
“Boti hizi ziongeze hamasa kwenu ya kuwa na umoja na mshikamano miongoni mwenu, ziweze kuwanufaisha na kuwaongezea kipato huku mkizingatia hifadhi ya mazingira”, Alisisitiza Dkt. Mkama
Alisema kuwa Ofisi ya Makamu wa Rais inaendeleza ushirikiano mzuri uliopobaina ya Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania (SJMT) na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar (SMZ) katika kutekeleza miradi ya maendeleo.
Pia, ameridhishwa na kasi ya uchimbaji wa visima sita na ujenzi wa minara ya matanki ya maji kwa ajili ya matumizi ya nyumbani na kilimo cha mbogamboga kwa wakazi wa Shehia 3 za Matemwe - Kijini, Matemwe Mbuyutende na Matemwe Jugakuu.
Nae Mratibu wa Mradi huo kutoka Ofisi ya Makamu wa Rais, Dkt. James Nyarobi amesema maeneo ya Mradi yamechaguliwa kwa kuzingatia maeneo kame yenye jamii za wakulima, wafugaji na wavuvi kwa lengo la kuongeza uwezo wa kuhimili mabadiliko ya tabianchi katika jamii za vijijini kwa kuimarisha mifumo ikolojia na shughuli mbadala za kujiongezea kipato.
Tanzania ni miongoni mwa nchi zinazoathiriwa na mabadiliko ya tabianchi katika sekta mbalimbali za uzalishaji nchini ikiwemo sekta za Kilimo, Mifugo, Maji, Nishati, Maliasili, Miundombinu na Usafirishaji ambapo jamii maskini hasa za vijijini huathiriwa zaidi na mabadiliko haya. Hivyo mradi wa EBARR unalenga kusaidia jamii kukabiliana na athari za mabadiliko ya tabianchi na kuboresha maisha yao.
Katika kukabiliana na athari za mabadiliko ya tabianchi, Serikali kupitia Ofisi ya Makamu wa Rais inaratibu utekelezaji wa Mradi wa Kuhimili Mabadiliko ya Tabianchi kwa kutumia Mifumo ikolojia Vijijini wenye thamani ya Shilingi za kitanzania Bilioni 17 ikiwa ni ufadhili wa Mfuko wa Mazingira Duniani (GEF). Mradi huu unatekelezwa katika Wilaya tano nchini, ambazo ni Simanjiro, Kishapu, Mvomero, Mpwapwa na Kaskazini A Unguja.