Na Beatrice Lyimo-MAELEZO, Dodoma
Serikali imeitaka Manispaa ya Kigoma Ujiji kutekeleza uamuzi wa Serikali Kuu wa kujiondoa kwenye Mpango wa Uendeshaji wa Shughuli za Serikali kwa Uwazi(OGP) la sivyo hatua kali za kisheria zitachukuliwa.
Agizo hilo limetolewa na Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora George Mkuchika leo mjini Dodoma wakati akijibu swali la nyongeza la Mbunge wa Kigoma Mjini Mhe. Kabwe Zitto kuhusu uhalali wa manispaa ya Kigoma Ujiji kuendelea kutekeleleza mpango huo.
Waziri Mkuchika amesema kuwa Mpango wa OGP ni wa hiari ambapo nchi inaweza kujiunga baada ya kutimiza masharti na hata kujitoa bila kuwepo na kizuizi chochote.
"Baada ya Serikali kushiriki utekelezaji wa Mpango kwa zaidi ya miaka minne imeamua kujitoa, Tanzania sio nchi pekee iliyojiunga na mpango huo na kisha kujitoa, nchi nyingine kama vile Hungary na Urusi zilijiunga na baadae kujitoa" ameongeza Waziri Mkuchika.
Waziri Mkuchika ameongeza kuwa endapo Manispaa ya Kigoma Ujiji haitatekeleza agizo hilo, hatua kali za kisheria zitachukuliwa dhidi ya Manispaa hiyo ikiwemo kuvunjwa kwa Baraza la Madiwani.
Aidha, amesema kuwa, Serikali ya Tanzania tangu kupata uhuru imekuwa na mashirikiano ya kikanda na kimataifa katika kutekeleza falsafa ya uwazi na uwajibikaji.
Hata hivyo, Waziri Mkuchika amewahakikishia Watanzania kuwa uamuzi wa Tanzania kujitoa katika Mpango huo hauna madhara yoyote kwani mipango inayotekelezwa ndani ya nchi inajitosheleza kuendeleza na kuimarisha misingi ya uwazi, uwajibikaji na mapambana dhidi ya rushwa.