Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Blogu ya Idara ya Habari - MAELEZO

Serikali Yaendelea Kuutangaza Mlima Kilimanjaro Kimataifa
Feb 10, 2022
Na Jacquiline Mrisho

Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii, Mhe. Mary Masanja, amesema Serikali imeendelea kufanya jitihada mbalimbali za kuutangaza mlima Kilimanjaro Kimataifa ili kukuza utalii katika mlima huo.

Ameyasema hayo Bungeni jijini Dodoma alipokuwa akijibu swali la Mbunge wa Viti Maalum, Ester Maleko aliyetaka kujua mikakati ya Serikali ya kukuza utalii wa Mlima Kilimanjaro.

Amesema Serikali kwa kushirikiana na wadau imekuwa ikitangaza Mlima Kilimanjaro kwa kufanya Onesho la Utalii la Kimataifa la Kilifair linalofanyika mwezi Juni mkoani Kilimanjaro na mbio za Kilimanjaro zinazofanyika mwezi Februari ya kila mwaka.

Ameongeza kuwa, Serikali imeshiriki katika Makongamano ya Kimataifa ikiwemo World Travel Market-London, Internationale Tourismus-Börse-Ujerumani, Fitur-Hispania na Expo 2020 Dubai lengo likiwa ni kutangaza vivutio vya utalii vilivyoko nchini Tanzania pamoja na kuutangaza mlima Kilimanjaro.

Pia, Serikali imekuwa ikishiriki katika makongamano ya Kimataifa yanayolenga kuimarisha uhifadhi na kutangaza utalii wa Mlima Kilimanjaro mfano Kongamano la Milima Mirefu Duniani (International Moutains Alliance-ITA).

Aidha, Serikali imeandaa  na kushiriki  katika Onesho la Kwanza la Kimataifa la Utalii la Jumuiya ya Afrika Mashariki (East Africa Regional Tourism Expo-EARTE)  lililofanyika jijini Arusha.

Mhe. Masanja ameweka bayana kuwa Mlima Kilimanjaro ni moja ya eneo la urithi wa dunia hivyo kupitia mikutano mbalimbali ya UNESCO mlima huo hutangazwa.

Vilevile, amefafanua kuwa Serikali imekuwa ikitangaza Mlima Kilimanjaro kupitia watalii wanaotembelea maeneo mbalimbali ya vivutio nchini Tanzania ambao huwa mabalozi wa kuutangaza mlima huo.

Amesema Serikali itaendelea kutumia matukio muhimu ya kitaifa kama sherehe za uhuru kuhamasisha jamii kupanda mlima Kilimanjaro.

Mipangilio
Marekebisho ya Mandhari
Marekebisho ya Maandishi