Na Immaculate Makilika - MAELEZO
Serikali imeendelea kutoa msamaha wa kodi kwa baadhi ya bidhaa zinazozalishwa ndani ya nchi na kutoza kodi zaidi kwenye bidhaa zinazoingia nchini ili kuhakikisha bidhaa za wazalishaji wa ndani zinalindwa.
Akizungumza Bungeni leo jijini Dodoma, Naibu Waziri wa Viwanda na Biashara, Injiania Stella Manyanya alisema kuwa Serikali imeendelea kutoa msamaha wa kodi kwa baadhi ya bidhaa zinazozalishwa ndani ya nchi na kutoza kodi zaidi kwenye bidhaa zinazoingia nchini katika kiwango cha asilimia 10 kwa bidhaa ghafi na asilimia 25 kwa bidhaa zilizo tayari kutumiwa na mlaji, ambapo viwango hivyo vinavyoweza kutozwa zaidi ya asilimia 25 kulingana na umuhimu wake.
Naibu Waziri huyo, Injiania Manyanya alisema, “Kwa mfano katika mwaka 2018/19 Serikali iliongeza kodi kati ya asilimia 25 hadi 35 kwenye mafuta ya kula yanayoingizwa nchini”
Aidha, aliongeza kuwa ili kulinda wazalishaji wanaotumia malighafi za ndani Serikali imeongeza kodi kwa bidhaa zinazotoka nje, kwa mfano mvinyo wa zabibu ulioingizwa toka nje ya nchi kutoka shilingi 2,349 hadi 2,466 kwa lita wakati unaozalishwa ndani ukitozwa shilingi 200 tu kwa lita.
Mikakati ya Serikali ya kulinda biashara za wazalishaji wa ndani ili kuwajengea uwezo kuelekea uchumi wa viwanda ni udhibiti na usimamizi maalum kwa kutoa vibali na leseni kwa baadhi ya bidhaa zinazoingizwa nchini kama vile sukari, maziwa ya mtindi, mitumba na magunia au viroba vya kufungashia bidhaa.
Kuimarisha Vituo vya Pamoja Mipakani (One Stop Boarder Post –OSBP), katika maeneo ya kuingiza bidhaa nchini, ambapo udhibiti na ukaguzi katika viwanja vya ndege na bandari umeimarishwa ili kudhibiti bidhaa za magendo hafifu na bandia kuingizwa nchini.
Injiania Manyanya alisema kuwa pamoja na mikakati ya kisera, kisheria na kiutendaji, Serikali imeendelea kuwawekea mazingira wezeshi wafanyabiashara wa ndani ili waweze kuzalisha bidhaa zenye ushindani katika soko.
Vilele Serikali imeandaa na kutekeleza Mpango wa Kuboresha Mfumo wa Udhibiti wa Biashara nchini, kuanzisha Vituo vya ushauri wa Biashara ili kutatua changamoto zinazowakabili, na vituo vya ushauri wa kodi ambavyo vinatoa elimu kuhusu namna bora ya kuanzisha na kufanya biashara na aina ya kodi zinazohusiana na kila aina ya biashara nchini.