Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Blogu ya Idara ya Habari - MAELEZO

Serikali Yadhamiria Kuweka Misingi Thabiti Katika Kuimarisha Upatikanaji wa Haki – Katibu Mkuu Makondo
Sep 26, 2022
Na Jacquiline Mrisho

Serikali ya Tanzania imedhamiria kuweka misingi thabiti ya kisera na kiutawala katika kuimarisha upatikanaji wa haki jinai nchini.

Hayo yamesemwa na Katibu Mkuu Wizara ya Katiba na Sheria, Bi. Mary Makondo wakati akifungua kikao cha Wakuu wa Taasisi cha kupokea maoni kuhusu rasimu ya Sera ya Taifa ya Mashtaka ya mwaka 2022 leo tarehe 26, Septemba 2022 mkoani Singida.

Bi. Makondo amesema Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania imekuwa ikifanya maboresho katika mifumo ya Haki Jinai, maboresho hayo yanalenga kuimarisha mifumo ya kiutawala na kiutendaji katika kuendesha mashauri ya jinai nchini.

‘’Matokeo ya maboresho hayo ni kuongezeka kwa ufanisi katika kuratibu na kusimamia uendeshaji wa mashauri nchini ikiwa na madhumuni ya kuwa na mfumo thabiti  wa uendeshaji wa mashauri ya jinai ili haki ipatikane kwa mtu anayestahili’’, ameongeza Bi. Makondo

Mbali na hayo, Bi. Makondo amesema kutokuwepo kwa Sera ya Taifa ya Mashtaka inayotoa miongozo katika uendeshaji wa mashtaka kumesababisha athari mbalimbali ikiwemo mlundikano wa mahabusu, ugumu wa kubaini mbinu za makosa makubwa ya jinai na kutokuwa na mfumo madhubuti wa usimamizi wa mashauri.

Vilevile, Bi. Makondo ameongeza ‘’Kwa kutambua hilo, Serikali kwa kushirikiana na Wadau wa Haki Jinai wameandaa Rasimu ya Sera ya Taifa ya Mashtaka ili kuwezesha kuimarisha huduma jumuishi za uendeshaji wa mashauri ya jinai nchini ili kufanikisha uwepo wa amani na usalama katika jamii’’.

Awali akimkaribisha Katibu Mkuu kufungua kikao hicho, Kaimu Mkurugenzi wa Sera na Mipango, Bw. Emmanuel Mayeji amesema Serikali ya Tanzania imekuwa ikifanya maboresho katika kuimarisha uendeshaji wa mashauri nchini, maboresho makubwa yaliyofanyika ni pamoja na kuanzisha Ofisi ya Taifa ya Mashtaka mwaka 2018.

Aidha, Bw. Mayeji aliongeza kuwa maboresho hayo yalilenga kuimarisha mifumo ya kiutawala na kiutendaji wa kuendesha mashauri ya jinai.

Mipangilio
Marekebisho ya Mandhari
Marekebisho ya Maandishi