Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Philip Mpango amesema Serikali ya Awamu ya Sita ina dhamira ya dhati kuhakikisha huduma bora za afya zinasogezwa jirani na wananchi.
Makamu wa Rais amesema hayo wakati wa hafla ya uzinduzi wa huduma za mashine ya MRI katika Hospitali ya Rufaa ya Kanda Mbeya iliogharimu shilingi bilioni 3. Amesema kusogezwa kwa huduma bora kama uwepo wa MRI katika hospitali hiyo ni lengo la kuwapunguzia wananchi gharama na adha za kufuata huduma hizo maeneo ya mbali.
Makamu wa Rais ameupongeza uongozi na wahudumu katika hospitali hiyo kwa kuendelea kujitoa katika kuwahumia wananchi na ubunifu walioufanya katika kutafuta vifaa mbalimbali ikiwemo vya kusafirisha wagonjwa ndani ya hospitali.
Aidha, ametoa wito kwa uongozi wa Hospitali ya Rufaa ya Kanda Mbeya kuzingatia utunzaji wa MRI hiyo ikiwemo kuzingatia muda maalumu wa matengenezo uliopangwa ili itoe huduma kwa muda mrefu.
Pia, ameagiza Wizara ya Afya kukamilisha utaratibu unaopaswa ili kuifanya Hospitali hiyo kuwa taasisi na kujiendesha kiufanisi zaidi.
Kwa upande wake Naibu Waziri wa Afya, Dkt. Godwin Mollel amesema wabunifu katika Hospitali ya Rufaa ya Kanda Mbeya wako katika hatua za mwisho kutengeneza kifaa maalum kinachowekwa mkononi kwa mgonjwa kitakachoweza kutuma ripoti kwa Daktari muda wote juu ya hali ya mgonjwa inavyobadilika hata akiwa mbali na hospitali.
Amewapongeza wabunifu katika hospitali hiyo kwa kutumia rasilimali ziliozopo kubuni masuluhisho mbalimbali kwa lengo la kutoa huduma bora hospitalini.