Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Blogu ya Idara ya Habari - MAELEZO

Serikali Yaanza Kuboresha Mashamba ya Mifugo
Nov 19, 2022
Na Jacquiline Mrisho

Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Mhe. Mashimba Ndaki (Mb) amesema Serikali imeanza kuboresha mashamba yake ya mifugo kwa kununua ng'ombe kwa ajili ya kuongeza uzalishaji na kuuza kwa watu binafsi.

Waziri Ndaki amesema hayo (18.11.2022) wakati wa hafla fupi ya kukabidhi ng'ombe 1,160 wenye thamani ya Shilingi bilioni 2.9 iliyofanyika katika Shamba la Kuzalisha Mifugo la Mabuki lililopo Wilaya ya Misungwi mkoani Mwanza, ambapo Shamba la Mabuki limekabidhiwa ng'ombe 500, Shamba la Sao Hill lililopo mkoani Iringa ng'ombe 500 na Shamba la Kitulo lililopo mkoani Mbeya ng'ombe 160.

Mhe. Ndaki amesema lengo la kugawa ng’ombe hao jike ambao hawajazaa (mitamba) ni kuhakikisha wafugaji wanapata mifugo ambayo itakuwa na tija kwa maana ya kuwa na nyama ya kutosha pamoja na maziwa.

"Tutaendelea kugawa mitamba katika bajeti zijazo ili mashamba yetu yote ya Serikali yaweze kuwa na mitamba inayotosha ili wafugaji wetu wakitaka kuchukua ili wakabadilishe aina ya ngo'mbe tunayofuga Tanzania waweze kupata kiurahisi" amesema Mhe. Ndaki.

Aidha, ameongeza kuwa wizara inatarajia kuzindua ugawaji wa mitamba hiyo katika Wilaya ya Chamwino mkoani Dodoma pamoja na kugawa mitamba kwenye wilaya zaidi ya kumi ili iende kwa watu binafsi na vikundi mbalimbali vya wafugaji, nia ni kubadilisha aina ya mifugo iliyopo na kuwa na aina iliyoboreshwa itakayotoa tija kubwa kwenye mazao ya mifugo.

"Tunamshukuru pia Mhe. Rais Samia Suluhu Hassan katika kufanya mageuzi kwenye sekta ya Mifugo" Amesema Mhe. Ndaki.

Akimwakilisha Mkurugenzi wa Idara ya Uzalishaji na Masoko kutoka Wizara ya Mifugo na Uvuvi, Mkurugenzi Msaidizi wa Uzalishaji wa Mifugo, Bw. Simon Lyimo amesema malengo makuu ya mkakati huu ni kutumia madume bora ya ng’ombe yatakayoongeza tija kwa ng’ombe wa asili waliopo nchini.

Amesema kutakuwa na kampeni kubwa nchini ya kuhamasisha wafugaji kupandikiza mifugo yao mimba kwa njia ya chupa (uhimilishaji) ili kupata matokeo bora ya mifugo itakayozaliwa kwa kutumia mbegu bora za madume ya mifugo.

Kuhusu malisho ya mifugo, amesema kutakuwa na mkakati wa uwepo wa mashamba darasa katika maeneo mbalimbali nchini pamoja na uchimbaji wa mabwawa kwa ajili ya kunyweshea mifugo maji.

Naye Meneja wa Shamba la Kuzalisha Mifugo la Mabuki mkoani Mwanza, Bi. Lini Mwalla ameishukuru Wizara ya Mifugo na Uvuvi kwa kuwezesha kuwapatia mitamba hiyo kwani haijawahi kutokea kupatiwa ng'ombe wengi kama hao kwenye shamba hilo.

Bi. Mwalla amesema uongozi wa shamba hilo utahakikisha unasimamia vyema ng’ombe hao ili waweze kuwa bora zaidi na kuongeza tija kwa watu binafsi ambao huwa wanataka kununua kwa kuwa shamba hilo limekuwa likipokea maombi mengi ya watu kutaka kununua ng’ombe lakini shamba halikuwa na ng’ombe wa kutosha.

Mipangilio
Marekebisho ya Mandhari
Marekebisho ya Maandishi