Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Blogu ya Idara ya Habari - MAELEZO

Serikali Yaamua Kuinua Zao la Kahawa Nchini
Feb 06, 2019
Na Msemaji Mkuu

Na Beatrice Lyimo-MAELEZO

DODOMA

Serikali imeamua kuanzisha minada ya kahawa kwenye maeneo ya uzalishaji kuanzia msimu wa 2019/2020 ili kuinua zao hilo la kimkakati nchini.

Hayo yamesemwa leo Bungeni Dodoma na Naibu Waziri wa Kilimo,  Omary Mgumba wakati akijibu swali Mhe. Bernadeta Mushashu kuhusu mpango wa Serikali wa kuinua zao la kahawa Mkoani Kagera ikiwemo kupandisha bei ili kumnufaisha mkulima.

Mgumba amesema kuwa lengo la utaratibu huo ni kuharakisha malipo na kuongeza ufanisi katika usimamizi wa minada na kuwashirikisha wakulima wengi zaidi katika mikoa inayozalisha kahawa ikiwemo Mkoa wa Kagera.

Aidha, amesema kuwa katika kuboresha mazingira ya biashara ya zao hilo, Serikali inadhibiti makato yasiyo ya tija kwa wakulima yanayokatwa kwenye Vyama Vikuu vya Ushirika na Vyama vya Msingi ili kubaki na makato yanayolenga kuendeleza zao la kahawa.

"Kupitia Benki ya Maendeleo ya Kilimo(TADB), Serikali imewezesha vyama vya ushirika vya kahawa kupata mikopo yenye riba nafuu kwa ajili ya kufanikisha shughuli za ukusanyaji na uuzaji wa kahawa ya wakulima hivyo kumpunguzia mkulima mzigo wa riba uliokuwa unatozwa na mabenki ya kibiashara," amefafanua Naibu Waziri Mgumba.

Hata hivyo,  Mgumba ameongeza kuwa, Serikali imefuta tozo na kupunguza viwango vya makato mbalimbali vilivyokuwa vinatozwa kwa wakulima ikiwa ni pamoja na kupunguza tozo zilizokuwa zinatozwa katika biashara ya kahawa pamoja na kupunguza viwango vya makato mbalimbali vilivyokuwa vinakusanywa na mkulima.

"Serikali pia  imepunguza kiwango cha ushuru wa mazao unaotozwa na Mamlaka za Serikali za Mitaa kutoka asilimia tanohadi asilimia tatuya bei ya kahawa shambani," amesema Mgumba

Wakati huo huo,  Naibu Waziri wa Kilimo, Mhe. Innocent Bashungwa akijibu swali la Mbunge wa Ziwani, Mhe. Nassoro Omar kuhusu mpango wa Serikali kuhamasisha kilimo cha viungo vya chakula nchini amesema kuwa, Serikali inatambua umuhimu wa mazao hayo  kutokana na mchango wake katika kipato cha mkulima mmoja mmoja na pia katika kuliingizia Taifa fedha za kigeni.

"Kutokana na umuhimu huo, Serikali kwa kushirikiana na Sekta binafsi imeandaa mkakati wa kuendeleza mazao ya viungo (Spice Sub-Sector Strategy-2014) ambao unalenga kuongeza uzalishaji na tija ukiwa na maeneo mahususi ya utoaji mafunzo ya kuongeza ujuzi katika uzalishaji kwa wataalamu wa wakulima, uanzishaji wa vituo vya kukusanyia mazao na kupanga madaraja na kuunda masoko ya pamoja ya wakulima," amefafanua Naibu Waziri Bashungwa.

Ameongeza kuwa, Serikali imeandaa Mwongozo wa uzalishaji wa mazao ambao umeainisha maeneo yanayofaa kwa uzalishaji wa mazao mbalimbali yakiwemo ya viungo ambao umalenga kuonesha fursa za uzalishaji wa mazao hayo.

Zao la kahawa ni moja ya mazao ya kimkakati yanayoliingizia Taifa fedha zakigeni sambamba na korosho, pamba na chai. 

(Picha na Idara ya Habari-MAELEZO)

Mipangilio
Marekebisho ya Mandhari
Marekebisho ya Maandishi