Na Mwandishi Wetu - WUSM
Katibu Mkuu Wizara ya Utamaduni, Sanaa na Michezo, Dkt. Hassan Abbasi amezindua kampeni maalum ya #MARA100ZAIDI ya kampuni ya Star Times kupitia ving'amuzi vyake ambayo imesheheni vipindi na chaneli mbalimbali ndani yake za kuonesha kazi za sanaa, michezo na utamaduni.
Dkt. Abbasi amefanya uzinduzi huo usiku wa Januari 6, 2022 katika Hoteli ya Serena jijini Dar es salaam.
Akizungumza kwa niaba ya Wizara na Serikali kwa ujumla katika uzinduzi huo, Dkt. Abbasi amewapongeza Star Times kwa kuanzisha chaneli mpya maalum kwa ajili ya kuonesha maudhui kutoka Tanzania pekee iitwayo ST Bongo.
Amesema mwaka huu 2022 Serikali chini ya Rais Samia Suluhu Hassan na Wizara wamejipanga kufanya mambo mengi makubwa ikiwemo kutoa mirabaha kwa wasanii, kuimarisha Mfuko wa Maendeleo ya Sanaa na Utamaduni na kuwataka wadau kutimiza wajibu wao.
Ameongeza kuwa wadau wa sanaa hatuna budi kumuombea Rais wetu Mhe. Samia Suluhu Hassan dua njema kwani ametenda makubwa katika sanaa na michezo mwaka 2021 ili azidi kuwatendea mema zaidi Watanzania na mengi zaidi katika tasnia za ubunifu na burudani.