Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Blogu ya Idara ya Habari - MAELEZO

Serikali Yaahidi Kuendelea Kufungua Matawi ya TADB
Sep 19, 2022
Na Jacquiline Mrisho


Na. Hilda Mlay (TIA)

Serikali imeeleza kuwa Benki ya Maendeleo ya Kilimo nchini (TADB) itaangalia uwezekano wa kufungua matawi katika mikoa na wilaya baada ya kukamilisha ufunguzi wa matawi hayo katika kanda.

Hayo yameelezwa na Naibu Waziri wa Fedha na Mipango, Mhe. Hamad Hassan Chande (Mb) alipojibu swali la Mbunge wa Viti Maalum, Mhe. Oliver Daniel Semuguruka aliyetaka kujua wakati ambao Serikali itafungua matawi ya Benki ya Kilimo katika Wilaya za Mkoa wa Kagera.

Mhe. Chande alisema kuwa ufunguaji wa matawi hayo utategemea uwezo wa benki hiyo wa kifedha ikiwa ni pamoja na faida na ukuaji wa mtaji.

Alisema benki hiyo imefanikiwa kufungua matawi katika kanda 5 ambazo ni; kanda ya kati – Dodoma, kanda ya Mashariki – Dar es salaam, kanda ya Magharibi – Tabora, nyanda za juu Kusini – Mbeya na kanda ya ziwa – Mwanza ambayo inahudumia mkoa wa Kagera na wilaya zake.

“Aidha, benki ipo katika hatua za mwisho za kufungua ofisi ya Kanda ya Kusini – Mtwara na hatua za awali za kufungua ofisi ya Kanda ya Kaskazini - Arusha”, alibainisha Mhe. Chande.

Wakati huo huo alieleza kuwa kuanzia 2021 Benki Kuu ya Tanzania (BoT) ilianzisha mkopo maalum wa Shilingi trilioni 1.0 kwa benki na taasisi za kifedha ili kuziwezesha kutoa mikopo kwenye sekta ya kilimo ikiwemo mifugo, uvuvi na misitu.

Alieleza hayo alipokuwa akijibu swali la Mbunge wa Mbeya Vijijini, Mhe. Oran Manase Njeza, aliyetaka kujua mikakati ya Serikali ya kutumia mfuko uliopo BoT wa Shilingi trilioni moja kutoa dhamana kwa waagizaji mbolea kwa njia ya Hedging /Options.

Mhe. Chande alisema kupitia mkopo huo mkopaji anaruhusiwa kununua au kuagiza mbolea na pembejeo za kilimo kwa utaratibu atakaoona unafaa ikiwemo hedging na options.

Vilevile, Mhe. Chande, alisema kuwa katika kipindi cha miaka mitatu iliyopita (2019/20 – 2021/22), thamani ya mikataba ya mikopo kutoka vyanzo vya nje iliyosainiwa kwa ajili ya utekelezaji wa miradi ya Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar (SMZ) ikiwemo barabara, afya, elimu na mapambano dhidi ya janga la UVIKO-19 ni takribani shilingi trilioni 1.1.

Alisema kuwa kwa mujibu wa kifungu cha 15 cha Sheria ya Mikopo, Dhamana na Misaada Sura 134, Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar imepewa mamlaka ya kupokea misaada yenyewe kutoka kwa Washirika wa Maendeleo.

“Kwa mujibu wa kifungu cha 3 na 13, mamlaka ya kukopa na kutoa dhamana yamewekwa chini ya Waziri wa Fedha wa Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na anaweza kuyakasimu kwa Waziri wa Fedha wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar baada ya kushauriwa na Kamati ya Kitaifa ya Madeni yenye wajumbe toka pande zote za Muungano” alifafanua Mhe. Chande.

Mipangilio
Marekebisho ya Mandhari
Marekebisho ya Maandishi