Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Abdallah Ulega amesema Serikali inayoongozwa na Rais Samia Suluhu Hassan imejipanga kupeleka miradi ya maendeleo ya ufugaji Kuku, Mbuzi na Samaki katika Wilaya ya Ruangwa ili iwasaidie kuinua Uchumi wao.
Ulega aliyasema hayo wakati akiongea na Viongozi wa Wilaya ya Ruangwa iliyopo Mkoani Lindi Septemba 22, 2021.
Alisema kutokana na kasi kubwa ya maendeleo ya Wilaya hiyo inayochochewa na shughuli za uchimbaji madini Serikali imeona ni vyema kupeleka miradi hiyo kwa kina mama na vijana ili kukuza uchumi wao na kukidhi mahitaji ya mazao ya Mifugo katika Wilaya hiyo.
Naibu Waziri Ulega aliitaja miradi hiyo ambayo itapelekwa katika Wilaya hiyo na kuwasaidia wakina mama na vijana ni pamoja ufugaji wa kuku na ufugaji wa Samaki na Mradi wa Kopa mbuzi lipa mbuzi.
"Mwezi Oktoba tutaanza na Vikundi kumi, tutaleta Wilayani hapa kuku elfu mbili (2000) ikiambatana na semina ya kuelekeza namna ya kufuga kuku hao kibiashara," alisema Ulega
Aidha, Waziri Ulega alimuagiza Mkuu wa Wilaya ya Ruangwa, Hassan Ngoma kutafuta eneo zuri ambalo watalitumia kuanza kufanya ufugaji wa Samaki.
"Sasa tafuteni eneo na kikundi kimoja kizuri ili tuje kuweka shamba darasa la ufugaji wa samaki, kikundi hicho kitakuwa kinavuna Samaki hao na watawafundisha na wengine kuhusu ufugaji huo wa samaki," aliongeza Ulega
Waziri Ulega alimuahidi Mkuu wa Wilaya hiyo kuwa atapeleka wataalamu wa shughuli ya ufugaji wa Samaki ili kuwasaidia wananchi hao.
Naye Mkuu wa Wilaya hiyo, Hassan Ngoma alisema kuwa kufuatia kuchipuka kwa shughuli za madini Wilayani humo kumepelekea kuongezeka kwa mahitaji mbalimbali muhimu ikiwemo mahitaji ya nyama, mayai, Samaki na maziwa ambayo mengi yamekuwa yakiagizwa katika maeneo mengine ya nchi na hivyo alimuomba Naibu Waziri kuona hizo fursa na kuwawezesha wananchi wa Wilaya hiyo ili waweze kuzitumia.