Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Blogu ya Idara ya Habari - MAELEZO

Serikali ya Awamu ya Tano Imejikita Kutoa Huduma kwa Wananchi
Nov 09, 2017
Na Msemaji Mkuu

Na: Lilian Lundo – MAELEZO – Dodoma

Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Kassim Majaliwa amesisitiza kuwa Serikali ya Awamu ya Tano inayoongozwa na Rais Dkt. John Pombe Magufuli imejikitika katika kutaoa huduma kwa wananchi kama vile maji, elimu pamoja na afya.

Waziri Mkuu ametoa kauli hiyo leo Bungeni alipokuwa akijibu maswali ya papo kwa papo ambapo Mbunge wa Jimbo la Temeke (CUF) Abdallah Mtolea aliuliza mpango wa Serikali ya Awamu ya Tano juu ya mchakato wa kupata katiba mpya.

“Suala la katiba mpya lina gharama kubwa, kwa sasa Serikali ya awamu ya Tano imejikita kutoa huduma kwa wananchi ili kuwawezesha kuendelea na maisha,” alisema Waziri Mkuu.

Aliendelea kwa kusema, kwa sasa watanzania wanauhitaji mkubwa wa huduma za afya, maji na elimu hivyo Serikali imejikita zaidi katika kihakikisha kuwa wananchi wanapata huduma hizo.

Majaliwa amesema kuwa, katiba inayotumika sasa itaendelea kutumika mpaka hapo mapato yatakapotosheleza kutoa huduma kwa wananchi wakati huo huo kuruhusu mchakato wa katiba mpya.

Aidha alipokuwa akijibu swali la Kiongozi wa Kambi ya Upinzani Bungeni, Freeman Mbowe juu ya Serikali kuita wachunguzi kutoka nje ya nchi kwa ajili ya kuja kuchunguza wahalifu wa tukio la kushambuliwa kwa risasi kwa Mbunge wa Singida Mashariki Tundu Lissu.

Waziri Mkuu amesema kuwa, vyombo vya usalama vya ndani ya nchi vinauwezo wa kufanya uchunguzi juu tukio hilo, hivyo hakuna haja ya kuviita vyombo vya usalama kutoka nje ya nchi.

“Watu wanapofanya matukio ya uhalifu hufanya kwa kujificha hivyo hata kuwatambua ni lazima uchunguzi ufanyike kwa umakini. Tuvipe muda vyombo vyetu vya usalama, vitakavyomaliza uchunguzi vitatoa taarifa ya uchunguzi kwa familia ya Lissu na Watanzania,” alifafanua Waziri Mkuu.

Wakati huo huo, Waziri Mkuu amesema kuwa, Serikali imetenga Shilingi Bilioni 147 kwa ajili ya kulipa madeni ya watumishi wa umma na inaendelea kuwapindisha madaraja watumishi ambao hawajapandishwa madaraja kwa muda mrefu.

Mipangilio
Marekebisho ya Mandhari
Marekebisho ya Maandishi