Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Blogu ya Idara ya Habari - MAELEZO

Serikali, Watoa Huduma za Mawasiliano Waingia Maridhiano ya Kihistoria ya Shilingi Bilioni 50
Sep 25, 2023
Serikali, Watoa Huduma za Mawasiliano Waingia Maridhiano ya Kihistoria ya Shilingi Bilioni 50
Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Mhe. Nape Nnauye (kulia) leo Septemba 25, 2023, akishuhudia hafla ya utiaji saini Hati ya Maridhiano na Hati ya Mkataba wa Nyongeza Kwenye Miundombinu ya Mkongo wa Mawasiliano Kati ya Wizara hiyo na Umoja wa Watoa Huduma za Mawasiliano iliyofanyika katika Hoteli ya Serena Jijini Dar es Salaam.
Na Innocent Mungy

Katika hatua muhimu kwa Sekta ya Mawasiliano, Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania imesaini makubaliano muhimu ya maridhiano ya kihistoria na watoa huduma wakubwa wa mawasiliano leo yenye thamani ya Shilingi bilioni 50 kama malipo ya matumizi ya miundombinu tangu kujengwa kwake. Aidha, Watoa Huduma hao wameahidi kuwekeza Shilingi bilioni 32.5 katika maendeleo ya miundombinu zaidi nchini.

 

Hafla ya utiaji saini, iliyofanyika leo tarehe 25 Septemba 2023 jijini Dar es Salaam, ilikuwa ni hatua rasmi ya makubaliano kati ya Wizara ya Habari, Mawasiliano, na Teknolojia ya Habari na Muungano wa Watoa Huduma za Mawasiliano (Consortium of Telco Operators), ambao unajumuisha Kampuni za Airtel Tanzania, Honora Tanzania (Tigo), na Vodacom Tanzania.

 

Mhe. Nape Nnauye, Waziri wa Habari, Mawasiliano, na Teknolojia ya Habari, alitumia fursa hiyo kuonyesha shukrani zake za dhati kwa kukamilika kwa tukio hili kubwa. Alisisitiza umuhimu wa hafla hiyo, ambayo ilihusisha utiaji saini wa nyaraka mbili muhimu: Hati ya Maridhiano (Deed of Settlement) na Hati ya Mkataba wa Nyongeza (Addendum of Memorandum of Agreement) kati ya Serikali na Muungano wa Watoa Huduma za Mawasiliano.

Katika hotuba yake, Mhe. Nnauye alimshukuru na kumpongeza Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, kwa azma yake thabiti ya kukuza Sekta ya Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (ICT) nchini. Aidha Mhe. Nnauye alisisitiza dhamira ya Serikali katika kuhakikisha kwamba TEHAMA inakuwa kichocheo cha ukuaji wa kiuchumi nchini. Mhe. Nnauye pia alisema kuwa Serikali inaendelea kusimamia kwa karibu ili kuhakikisha huduma za Sekta ya TEHAMA zinawafikia Watanzania wote na kuwa wezeshaji wa ukuaji wa uchumi nchini.

 

Mhe. Nnauye alimpongeza Bw. Adolf Ndunguru, Katibu Mkuu wa Ofisi ya Rais - TAMISEMI, na Mwenyekiti wa Timu ya Serikali ya Majadiliano kwa uongozi wake wa kufanikisha kwa ufanisi mazungumzo haya mazito, akikiri mchango wa wajumbe wote wa timu hiyo na wataalamu wa serikali. Mhe. Nnauye pia alitoa shukrani zake kwa Bw. Mohammed Khamis Abdulla, Katibu Mkuu wa Wizara ya Habari, Mawasiliano, na Teknolojia ya Habari, kwa usimamizi wake bora katika kufikia makubaliano makubaliano haya muhimu kwa Sekta ya mawasiliano nchini.

 

Makubaliano haya ya kihistoria, yaliyoanza Oktoba 4, 2011, kati ya Serikali na Muungano wa Watoa Huduma za Mawasiliano, yalilenga kuimarisha miundombinu ya mawasiliano nchini. Yalijikita katika ujenzi wa Mtandao wa Optiki (Optic Fibre Cable Network) katika maeneo yaliyokuwa hayajafikiwa na mtandao wa Mkongo wa Taifa. Hata hivyo, utekelezaji wa makubaliano ulikumbwa na changamoto mbalimbali, ambazo zilipelekea majadiliano makubwa kati ya pande husika kuanzishwa.

Wakati wa hafla ya utiaji saini, Muungano wa Watoa Huduma ulikubaliana kutoa jumla ya Dola za Marekani milioni 20 kwa kipindi cha miaka mitano, sawa na takribani shilingi bilioni 50, kama malipo kwa matumizi ya miundombinu tangu kujengwa kwake. Aidha, wamekubali kuwekeza Dola za Marekani milioni 13, takribani shilingi bilioni 32.5, katika maendeleo ya miundombinu Zaidi ya Mawasiliano nchini.

 

Jambo jingine muhimu wakati wa hafla hiyo ilikuwa ni utiaji saini wa Hati ya Mkataba wa Nyongeza (Addendum of Memorandum of Agreement), ambayo iliingiza Kampuni ya Vodacom Tanzania kama mwanachama wa Muungano huo, ikionesha msisitizo wa ushirikiano kati ya Sekta Binafsi na Serikali katika kutoa huduma za mawasiliano kwa wananchi na kukuza ukuaji wa uchumi. Matokeo ya majadiliano haya yatawezesha Muungano wa Watoa Huduma hao kuhamisha takribani kilomita 3,000 za miundombinu ya mawasiliano kwa Serikali.

 

Waziri Nnauye alisisitiza dhamira ya Serikali ya kuimarisha upatikanaji na ubora wa huduma za mawasiliano nchini. Aliainisha hatua za hivi karibuni kama ujenzi wa minara ya mawasiliano 758 ili kupanua wigo wa huduma kwa zaidi ya Watanzania milioni nane na kupunguza gharama za ufungaji wa miundombinu ili kuharakisha utoaji wa huduma za mawasiliano unakuwa nafuu na bora zaidi.

Aidha, serikali imeongeza uwezo wa mtandao wa Mawasiliano wa Mkongo wa Taifa kutoka 200Gbps hadi 800Gbps, na ina mipango ya kuufikisha 2Tbps. Ujenzi wa Mtandao wa Mkongo wa Taifa unaendelea kujengwa na unatarajiwa kufikia wilaya 99 kati ya 139 ifikapo Machi mwakani 2024, na lengo la kufikia wilaya zote ifikapo mwishoni mwaka 2024.

 

Mhe. Nnauye alisisitiza kuwa kuimarisha sekta ya TEHAMA na mawasiliano kutachochea maendeleo ya kiuchumi, kukuza biashara, na kuongeza uchumi wa kidijitali kwa maendeleo ya kijamii. Lengo la serikali ni kuhakikisha kuwa 85% ya Watanzania wanapata intaneti ya kasi ifikapo 2025.

 

Mhe. Nnauye alitoa maelekezo kwa utekelezaji mzuri wa makubaliano hayo, akisisitiza umuhimu wa haraka katika kukamilisha Mkataba wa Uwekezaji. Pia aliwaomba Wizara, Shirika la Mawasiliano Tanzania (TTCL), na Muungano wa Watoa Huduma kuhitimisha Mkataba wa Haki ya Matumizi na kuhakikisha kuwa miundombinu ya Mawasiliano inatumika kwa ufanisi na usawa kama ilivyokusudiwa. Hali kadhalika Waziri aliwasihi watoa huduma wote wa mawasiliano kuendelea kuwekeza katika miundombinu ili kuwafikia wananchi, na kuendeleza dhamira ya serikali ya kuunda mazingira rafiki na yenye kuwawezesha watoa huduma wote ili kuchangia katika kufanikisha Tanzania ya kidijitali.

 

Hafla hii ya utiaji saini imepokelewa kwa shangwe na vigezo vyote vya kitaaluma vya pande zote mbili, na inaonyesha hatua muhimu kuelekea kuimarisha miundombinu ya mawasiliano Tanzania.

Mipangilio
Marekebisho ya Mandhari
Marekebisho ya Maandishi