Na Tiganya Vincent, RS-Tabora
SERIKALI ya Mkoa wa Tabora imesema itakamata mali za kampuni zitakazo sambaza mbegu mbovu kwa wakulima wapamba ili kufidia hasara itakayopatikana kutokana na mbegu kutoota au kuwa na dawa zisizoua wadudu waharibifu.
Kauli hiyo imetolewa hivi karibuni na Mkuu wa Mkoa wa Tabora wakati wa ziara yake ya kuwaelimisha wakulima wa pamba katika Wilaya ya Uyui.
Mkuu wa Mkoa alisema hawezi kukubali wakulima wapate hasara na yeye akiwa kiongozi anayebeba dhamana ya kuhakikisha kuwa anatumia vyombo vyote vinavyomsaidia na kumshauri katika kulinda maslahi ya umma wakiwemo wakulima wa pamba.
“Kampuni itakayo sambaza mbegu ambazo hazioti na dawa ambazo haziui wadudu nitamkamata yeye na mali zake zote ikiwemo magari na kupiga mahesabu ya hasara waliyopata wakulima na kisha nitamwaandikia invoice ili aweze kulipa gharama ya hasara hiyo ndio nitamwachia yeye na mali zao” alisema Mwanri.
Alisema kuwa hesabu hiyo itahusu kulipa fedha ambazo mkulima angepata kutokana na kilo ambazo angezalisha katika eneo lake na kwa kuzingatia bei ya ununuzi wa pamba wa wakati wa mauzo.
Kwa upande wa Meneja Mbegu kutoka Kampuni ya Usambazaji Mbegu ya Quoton Tanzania Limited, Phineas Chikaura alimuhakikishia Mkuu huyo wa Mkoa kuwa aina ya mbegu ni salama na kuwaomba wakulima kutochimba mashimo marefu wakati wa upandaji wa mbegu za pamba kwa sababu zao hilo halina nguvu za kusukuma udongo kama yalivyo mazao mengine.
Alisema kuwa wakichimba mashimo marefu upo uwezekano wa mbegu kushindwa kuotoa na kudai kuwa ni mbovu.
Chikaura aliongeza kuwa pia wakulima hawapaswi kuloweka mbegu za pamba kabla ya kupanda bali wanapaswa kugonja mvua inyeshe ndio wapande.
Alisema kuwa kitendo cha kuloweka wakati mwingine usababisha mbegu ishindwe kuotoa endapo mvua ikichelewa kunyesha katika eneo husika,