Na. Peter Haule, WFM, Dodoma
Waziri wa Fedha na Mipango, Mhe. Dkt. Mwigulu Lameck Nchemba, amefanya kikao naMwenyekiti Mwenza wa Washirika wa Maendeleo nchini, Mhe. Zlatan Milisic, kuhusu ushirikiano wa maendeleo na maandalizi ya mkutano kati ya Serikali na washirika hao utakaofanyika hivi karibuni.
Dkt. Nchemba amefanya kikao hicho jijini Dodoma na Mwenyekiti Mwenza wa Washirika wa Maendeleo nchini, Mhe. Zlatan Milisic, ambapo ajenda mbalimbali za mkutano huo ziliangaziwa.
Alisema kuwa miongoni mwa ajenda zitakazojadiliwa katika mkutano huo utakaofanyika hivi karibuni ni pamoja na kutengeneza mazingira bora ya uwekezaji, ajira kwa vijana, kukabiliana na mabadiliko ya tabia nchi na kilimo.
Ajenda nyingine ni kukuza uchumi, uhifadhi wa chakula, nishati kwa wote, uwezeshaji wa wanawake na utaratibu wa ushirikiano katika masuala ya kifedha katika utekelezaji wa miradi ya maendeleo.
“Mhe. Rais Samia Suluhu Hassan ametoa dira ya kukuza uchumi kwa kuwaleta wawekezaji na kuweka mazingira bora ya uwekezaji na biashara jambo ambalo pia linaendelea kutekelezwa kupitia wadau wa maendeleo”, alieleza Dkt. Nchemba.
Alisema kuwa Serikali kupitia Wizara ya Fedha na Mipango itaratibu ushiriki wa Wizara nyingine za kisekta kushiriki kikamilifu katika mkutano huo ili kuwa na manufaa makubwa kwa pande zote mbili.
Kwa upande wake Mwenyekiti Mwenza wa Washirika wa Maendeleo nchini, Bw. Zlatan Milisic, alisema washirika wa maendeleo wataendelea kushirikiana na Serikali ya Tanzania katika majadiliano yanayo hamasisha maendeleo ya wananchi katika kukuza mitaji, ajira na pia uwezeshaji wa wanawake.
Wadau wa maendeleo wameahidi kuendelea kudumisha ushirikiano na Tanzania katika masuala mbalimbali na kushiriki katika ukuzaji wa uchumi kwa manufaa ya pande zote.