Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Blogu ya Idara ya Habari - MAELEZO

Serikali Kuwekeza Miradi ya Kimkakati kwenye Makazi ya Wazee Nchini
Aug 26, 2022
Na Jacquiline Mrisho

Serikali kupitia Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum imejipanga kushirikiana na Wizara za kisekta na wadau mbalimbali ili kuboresha huduma katika Makazi ya Wazee nchini ikiwemo kutathimini matumizi ya ardhi na kuona fursa zilizopo kwa ajili ya kuanzisha miradi ya kimkakati kwenye maeneo hayo.

Hayo yamebainika wakati wa ziara ya Manaibu Makatibu Wakuu kutoka Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Ofisi ya Rais TAMISEMI, Wizara ya Uwekezaji, Viwanda na Biashara katika Makazi ya Wazee FungaFunga yaliyopo mkoani Morogoro.

Akizungumza wakati wa ziara hiyo, Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum, Amon Mpanju amesema kuwa, Serikali imekuja na mikakati ya kuwekeza miradi mbalimbali ya maendeleo na kuwataka wananchi wanaozunguka maeneo hayo kutovamia maeneo hayo ili yabaki yatumike kwa ajili ya kuhudumia Wazee.

Aidha, Mpanju amewasihi Wazee kujitokeza katika zoezi la Sensa ya Watu na Makazi ili kuwa na takwimu sahihi za Wazee zitakazosaidia Serikali kuweka mipango na mikakati kwa ajili ya kuwahudumia Wazee nchini.

Naye Naibu Katibu Mkuu Ofisi ya Rais TAMISEMI (Afya), Dkt. Grace Magembe amesema Wazee ni hazina na Serikali itaendelea kuwatunza na kuwahudumia ili kuhakikisha wanaishi katika amani na utulivu kwa kuwawekea mazingira salama.

Ameeleza kuwa suala la kuwatunza Wazee ni la jamii, hivyo jamii iwajibike kuwalea na kuwatunza Wazee na kuona jukumu hilo ni la Jamii nzima kwa kushirikiana na wadau. 

Kwa upande wake Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Uwekezaji, Viwanda na Biashara, Dkt. Hashir Abdalah amesema kuwa kwa upande wa Wizara hiyo itashirikiana na Wizara ya Maendeleo ya Jamii ili kuhakikisha maeneo ya Makazi hayo yanatumika katika kuanzisha miradi ya kimakakati.

Ameongeza kuwa, maeneo yaliyopo katika Makazi hayo yanaweza kutumika kwa ajili yakuwekeza katika miradi mbalimbali ya maendeleo kwa maslahi mapana ya kuwahudumia Wazee katika makazi hayo kutokana na mapato ya miradi hiyo.

Akitoa taarifa ya Makazi ya Wazee FungaFunga, Afisa Mfawidhi wa Makazi hayo, Rehema Kombe, amesema makazi hayo yanahudumia Wazee 21 kwa sasa ambao wanapatiwa huduma muhimu za malazi, chakula, huduma za afya na msaada wa Kisaikolojia kwa wazee hao.

Ameongeza kuwa makazi hayo mbali na kuwahudumia Wazee hao lakini lengo ni kuwa na mradi wa kulima mbogamboga ambapo inahusisha makazi hayo na wananchi wanazunguka eneo hilo ambapo ulimaji huo unawezesha kuzalisha mbogamboga kwa ajili ya Wazee na kuongeza kipato.

"Sisi kwetu ni mafanikio kuona Wazee wanaweza kufanya kazi nyepesi nyepesi kwa mfano kulima mbogamboga katika eneo hilo kwani inawasaidia kuchangamka na kuendelea na maisha", alisema Rehema. 

Wakizungumza katika ziara hiyo, Wazee wanaoishi katika Makazi ya Wazee FungaFunga wameishukuru Serikali kwa kutoa huduma ya muhimu katika makazi hayo.

Ziara hiyo imejumuisha wadau kutoka WHO, TASAF na wadau wengine wa maendeleo.

Mipangilio
Marekebisho ya Mandhari
Marekebisho ya Maandishi