Serikali imesema itaendelea kuwaunga mkono vijana nchini wanaobuni teknolojia mbalimbali zinazosaidia katika kutatua changamoto za mazingira zinazoikabili nchi yetu.
Hayo yamesemwa na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira), Mhe. Dkt. Selemani Jafo wakati akifungua Kongamano la Bunifu katika Mazingira na Mabadiliko ya Tabianchi lililofanyika jijini Dar es Salaam tarehe 25 Agosti, 2023.
Amesema changamoto za mazingira hasa ukame unayoyakabili baadhi ya maeneo nchini pamoja na usimamizi wa taka ngumu zinakwenda kutatuliwa kupitia vijana wanaojikita katika kubuni nyenzo rafiki wa mazingira.
Dkt. Jafo ametoa rai kwa vijana kutumia fursa ya kukusanya taka ngumu na kutengeneza bidhaa mbalimbali hatua itakayowapatia ajira na pia kusaidia katika shughuli ya utenganishaji wa taka.
“Tunaelezwa hapa, nchi yetu inazalisha mamilioni ya tani za taka ngumu kwa mwaka na kati ya hizo ni asilimia 30 tu ndizo zinaingia katika mfumo rasmi wa uchakataji hivyo teknolojia hizi vijana mlizobuni zitasaidia sana katika utunzaji wa mazingira, niwaombe muendelee kujikita katika teknolojia ya urejelezaji (recycling) ya taka,” alisema Mhe. Dkt. Jafo.
Aidha, Waziri Jafo aliwahimiza vijana kuchangamkia fursa ya Biashara ya Kaboni ili si tu kujipatia kipato bali pia kuunga mkono juhudi za Serikali katika kuhifadhi Mazingira kukabiliana na athari za Mabadiliko ya Tabianchi.
Aliweka wazi kuwa kupitia Kituo cha Taifa cha Kuratibu Kaboni (NCMC) hadi kufikia Julai 2023 tayari miradi 25 imekwishasajiliwa hivyo aliwahimiza vijana kuchangamkia fursa hiyo.
Halikadhalika Dkt. Jafo alitoa wito kwa Asasi ya Anza iliyoandaa Kongamano hilo kuendelea kuwasimamia vijana hao waweze kukua zaidi na waje kuonesha mafanikio makubwa zaidi katika teknolojia bunifu rafiki kwa mazingira.
Kwa upande wake Mkurugenzi wa Ubunifu na Teknolojia wa Tume ya Sayansi na Teknolojia (COSTECH), Bw. Gerald Kafuku alisema wanaendelea kuratibu, kuendeleza na kusaidia vijana katika teknolojia.
Alisema Tume inawasadia wabunifu kifedha na kiutaalamu ambapo imetoa shilingi bilioni 1.4 kwa wabunifu 37 na kuviwezesha vikundi vya ubunifu vitano kupitia programu maalumu iliyoianzisha.
Naye, Mkurugenzi Mtendaji wa Asasi ya Anza Bw. Joshua Elias alisema kuwa lengo la ubunifu huo ni kubadilisha taka ambazo zingeweza kuwa na athari za kimazingira na kuzibadilisha kuwa fursa.