Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Blogu ya Idara ya Habari - MAELEZO

Serikali Kutumia Bilioni 1 na Milioni 15 Kupeleka Mawasiliano Mbogwe
Jul 29, 2021
Na Jacquiline Mrisho

Na Faraja Mpina, MBOGWE

Serikali kupitia Mfuko wa Mawasiliano kwa Wote (UCSAF) inatarajia kutumia kiasi cha shilingi Bilioni 1,015,000,000 kufikisha huduma ya mawasiliano katika Wilaya ya Mbogwe iliyopo Mkoani Geita kupitia zabuni zilizotangazwa na Mfuko huo Juni 30 mwaka huu.

Hayo ameyazungumza Naibu Waziri wa Mawasiliano na Teknolojia ya Habari wakati wa ziara yake ya kukagua hali ya upatikanaji wa huduma ya mawasiliano katika wilaya hiyo ambapo alizungumza na uongozi wa Wilaya hiyo pamoja na wananchi na kuwahakikishia kuwa Serikali itawafikishia huduma ya mawasiliano kupitia bajeti ya mwaka huu wa fedha 2021/22

Mhandisi Kundo amesema kuwa ndani ya Wilaya ya Mbogwe, Minara mitano ya mawasiliano itajengwa na watoa huduma kupitia zabuni zilizotangazwa na UCSAF ili wananchi wa Wilaya hiyo waweze kupata huduma za mawasiliano kwa sababu mawasiliano yanasaidia kukuza uchumi, kuimarisha ulinzi na usalama na husaidia katika mazingira ya dharura

Ameongeza kuwa miongoni mwa maeneo yatakayofikishiwa huduma ya mawasiliano ni pamoja na kata ya Mbogwe ilipo ofisi ya Halmashauri ya Wilaya hiyo na ndipo jengo la ofisi mpya za Mkuu wa Wilaya linaendelea kujengwa lakini bado hakuna mawasiliano

Aidha, Mhandisi Kundo amesema kuwa Shirika la Mawasiliano Tanzania (TTCL) ambalo ndio linasimamia Mkongo wa Taifa wa Mawasiliano tayari limeshafikisha Mkongo  kwenye Ofisi za Halmashauri hiyo, hivyo mnara utakaojengwa katika kata ya Mbogwe utakuwa ni wa TTCL

Naye Mkuu wa Wilaya ya Mbogwe, Mhe. Mhandisi Charles Kabeho amesema kuwa maeneo mengi ya wilaya hiyo yana changamoto ya mawasiliano aidha kuwa na mawasiliano hafifu au kukosa kabisa mawasiliano hivyo ujenzi wa Minara mitano katika Wilaya hiyo itasaidia kutatua changamoto hiyo

Kwa upande wa Mbunge wa Mbogwe, Mhe. Nicodemas Maganga amesema kuwa anaishukuru Serikali kupitia Wizara ya Mawasiliano na Teknolojia ya Habari kwa kusikia kilio cha wananchi wa jimbo lake cha kuwapelekea huduma za mawasiliano kwa kupeleka ujenzi wa minara mitano ya mawasiliano katika maeneo yenye uhitaji mkubwa wa huduma hiyo

Katika Wilaya ya Mbogwe minara ya mawasiliano itajengwa katika vijiji vya Nyasato, Kasosobe, Ilolangulu, Iponya na ilipo Ofisi ya Mkurugenzi wa Halmashauri ya Mbogwe kupitia zabuni ya awamu ya sita ya Mfuko wa Mawasiliano kwa Wote.

Imetolewa na Kitengo cha Mawasiliano Serikalini

Wizara ya Mawasiliano na Teknolojia ya Habari

Mipangilio
Marekebisho ya Mandhari
Marekebisho ya Maandishi