Serikali imewahakikishia wadau wa Uchukuzi nchini kuwa itaendelea kufanyia kazi na kuchukua hatua za haraka changamoto mbalimbali zinazowasilishwa na wasafirishaji nchini na nchi jirani lengo likiwa ni kurahisisha huduma za usafiri na usafirishaji.
Akizungumza jijini Dar es Salaam na wadau wa usafirishaji katika kikao cha 16, Katibu Mkuu wa Uchukuzi Gabriel Migire amesema nchi jirani za Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, Uganda, Zambia, na Malawi zimekuwa zikisafirisha mizigo mbalimbali kupitia bandari ya Dar es Salaam, hivyo Serikali inafanya kila inaloweza kuhakikisha biashara inafanyika bila vikwazo.
“Tunashukuru kwenye suala la biashara ngazi zote za Serikali zimekuwa zikilitazama jambo hili kuanzia uongozi wa juu kwa ushirikiano mzuri sana lengo ni kuhakikisha kuwa malengo yote yaliyopangwa katika urahisishaji wa uingiaji na utoaji wa mizigo unazingatiwa”, amesisitiza Katibu Mkuu Migire.
Katibu Mkuu Migire amesema miongoni mwa matokeo chanya ya vikao vya mara kwa mara vya kusikiliza changamoto za wadau wa usafirishaji ni pamoja na kuongezeka kwa mchango wa bandari katika pato la Serikali ambapo limefikia asilimia 41 kutoka asilimia 38 kwa miezi michache iliyopita..
Aidha, Katibu Mkuu Migire amesisitiza umuhimu wa taasisi zilizopewa jukumu la kuunganisha mifumo ya TEHAMA kuharakisha zoezi hilo ili kupunguza adha kwa wasafirishaji wanaolazimika kupitia taasisi mbalimbali ili kupata vibali vya kuchukua mizigo yao inapowasili.
Naye Meneja wa Bandari ya Dar es Salaam, Mrisho Mrisho amesema kwa sasa Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari Tanzania (TPA) inafanyia kazi suala la kupunguza muda wa meli kupakia mizigo ili kuweza kuhudumia meli nyingi zaidi kwa wakati mmoja
Kwa upande wake Mwenyekiti wa Chama cha Madereva Tanzania (ITDA), Adam Mwenda ameipongeza Serikali kwa kuendelea kuwakutanisha wadau wa usafirishaji na kusikiliza changamoto mbalimbali walizonazo na kuzitafutia ufumbuzi kwa pamoja na kwa wakati.